Je, wewe ni mwenye furaha? Au hofu na hatia huondoa furaha yako yote? Je, ungetamani kuondoa hatia yako, lakini hujui kwa njia gani? Huenda unajiuliza, “Je, nitawahi kuwa mwenye furaha tena?”
Ninayo habari njema kwa ajili yako. Kuna Mmoja awezaye kukusaidia, kusamehe dhambi zako, na kukupa furaha ya daima. Jina lake ni Yesu. Ngoja nikuambie habari zake.
Mungu ndiye mwenyewe aliyeumba ulimwengu na vitu vyote vilivyomo. Alikuumba wewe na mimi.
Mungu anatupenda. Yeye humpenda kila mmoja ulimwenguni. Mungu anatupenda sana kiasi kwamba alimtuma Yesu Mwanawe pekee ulimwenguni. Yesu alipokuwa hapa duniani aliwaponya wagonjwa; aliwafariji wenye huzuni. Alifungua macho ya vipofu. Aliwafundisha watu mambo mengi. Tunasoma habari hii katika Biblia.
Yesu alitutaka tuelewe upendo mkuu alio nao Baba yake kwa ajili yako na mimi. Alitumia hadithi hii iliyoelezea upendo huo alio nao Baba yake:
Mtu mmoja aliishi kwake kwa furaha na vijana wake wawili. Alidhani yote ni salama. Siku moja, kijana wake mdogo aliasi na kumwambia, “Sipendi mji huu, nataka kufuata njia yangu mwenyewe na kuondoka. Nigawie urithi wangu.” Baba alihuzunika sana, lakini alimpa fedha na kumruhusu aende. Alijiuliza kama atawahi kumwona mwanawe tena. Kwa nini mwana alikuwa muasi hivyo?
Huyo kijana alienda mbali na akajifurahisha kwa hela yake na rafiki zake. Alifuja pesa zake na kufanya mabaya mengi. Alidhani amepata raha- hata kwa ghafla fedha zake ziliisha na rafiki zake walimwacha. Kisha, aliachwa mpweke na akajiona mwenye hatia sana. Je, angefanya nini?
Alimwendea mfugaji na alimpeleka kulisha nguruwe. Hakupewa chakula cha kutosha. Alikuwa na njaa sana hivyo alitamani kula hata takataka za nguruwe. Alianza kuwazia maovu yote aliyoyafanya na jinsi alivyomtendea vibaya baba yake. Alizidi kupata uchungu zaidi na kujuta.
Siku moja, alimkumbuka baba yake jinsi alivyokuwa mwenye upendo na jinsi alivyopendwa mwenye alipokuwa ingali nyumbani.
Alifikiri, “Je, ningeweza kurudi kwa baba yangu baada ya kumtendea haya yote? Je, bado angenipenda? Sistahili kuitwa mwanawe tena. Laiti angenipokea ningekuwa tu kama mfanyakazi wake nyumbani kwake!”
Kwa ghafla alisimama na kuanza safari ya kurejea nyumbani kwa baba yake. Ataona sasa kama bado angempenda au la.
Baba alimtamani kijana wake tangu alipotoka. Alijiuliza, “Je, mwanangu atarudi tena?” Siku moja alimwona mtu yuko mbali anakuja. “Je, anaweza kuwa mwanangu?” Alimkimbilia na kumkaribisha nyumbani kwa mikono ya ukarimu. Alisema, “Mwanangu huyu alipotea lakini sasa amepatikana.”
Sisi sote tumekuwa kama huyu kijana, sote tumetoka kwa Baba yetu wa mbinguni. Tumeharibu muda na mema yote ambayo ametukabidhi. Tumefanya maovu na kumwasi. Leo, Baba yetu wa mbinguni anatutaka tumrudie. Anatusubiria kwa mikono ya ukarimu.
Je, tunaelewa upendo alio nao Yesu kwa ajili yetu? Baada ya kufundisha hapa duniani kwa miaka mitatu, aliwaacha watu waovu wampigilie misumari msalabani. Alihisi maumivu na kukataliwa alipokuwa anajitoa na kumwaga damu yake kama sadaka kwa ajili ya dhambi za dunia nzima.
Tunapokwenda kwa Baba, tunamwomba atusamehe dhambi zetu. Anapotuona tumehuzunikia makosa yetu, anaamua yeye kutusamehe na kutusafisha udhalimu wetu wote kwa damu yake aliyomwaga. Jinsi gani tukio hili lilivyo safi! Yesu amekuwa Mwokozi wetu sasa. Tumezaliwa upya na kuwa mtu mpya. Uzima unao sasa kusudi jipya. Yesu amebadilisha hatia na hofu yetu kwa furaha na shangwe!