Yesu Rafiki Yako
Ninaye rafiki. Yeye ndiye rafiki bora ambaye nimewahi kujua. Yeye ni mwema sana na mkweli ambaye na wewe pia ningependa umfahamu. Jina lake ni Yesu. Cha kustajaabisha ni kwamba na yeye angependa awe rafiki yako.
Ngoja nikuambie habari zake. Tunasoma hadithi hii katika Biblia. Biblia ni kweli. Ni neno la Mungu. Mungu ndiye aliyeumba ulimwengu na vitu vyote vilivyomo. Yeye ni Bwana wa Mbinguni na dunia. Anatoa uzima na pumzi kwa viumbe vyote.
Yesu ni Mwana wa Mungu. Alitumwa na Mungu kutoka Mbinguni kuja duniani ili awe Mwokozi wetu. Mungu aliupenda ulimwengu sana (inamaanisha alikupenda wewe na mimi) hata akamtoa Mwanawe pekee, Yesu, (afe kwa ajili ya dhambi zetu) ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. (Yohana 3:16)
Yesu alikuja duniani kama mtoto mchanga. Baba na Mama yake wa hapa duniani walikuwa Yosefu na Maria. Alizaliwa katika zizi na kulazwa horini.
Yesu alikulia nyumbani kwa Yosefu na Maria, na aliwatii. Alikuwa na ndugu na dada wa kucheza nao. Alimsaidia Yosefu katika kazi yake ya useremala.
Yesu alipokuwa mtu mzima, aliwafundisha watu habari ya Baba yake wa Mbinguni. Aliwaonyesha upendo wa Mungu kwao. Aliwaponya wagonjwa na kuwafariji waliokuwa kwenye taabu. Alikuwa Rafiki ya watoto. Aliwakaribisha wasogee karibu naye. Alikuwa na muda kwa hao wadogo. Watoto walimpenda Yesu, na walipenda kuwa pamoja naye.
Baadhi ya watu hawakumpenda Yesu. Walimwonea wivu na hata kumchukia. Walimchukia sana, hata walitaka kumwua. Siku moja ya kutisha walimwua Yesu kwa kumpigilia misumari msalabani. Yesu hakufanya makosa. Ilimlazimu afe badala yetu kwa sababu wewe na mimi tumefanya makosa.
Hadithi ya Yesu haikomei pale penye kifo chake. Mungu alimfufua kutoka wafu! Wafuasi wake walimwona. Kisha siku moja alirudi mbinguni.
Leo anaweza kukuona na kukusikia. Yeye hujua yote juu yako na anakujali. Umwendee tu katika sala.
Mwambie shida zako zote. Yuko tayari kukusaidia. Unaweza kuongea naye kwa maombi, wakati wowote, popote pale.
Kuna siku atarudi tena! Wote wanaomwamini atawapeleka nyumbani, Mbinguni.