Kutambua Mbinu za Shetani kwa Kutumia Mwanga wa Neno la Mungu.
Lengo la Biblia Takatifu silo kuangalia hasa Shetani na kazi zake. Japokuwa tunapata mengi kwenye Biblia yanayofunua tabia zake na kazi zake.
Wakati fulani Shetani alikuwa malaika, lakini aligeuka kinyume cha Mungu, Muumba wake, na akatamani kuwa kama Mungu. Matendo ya ufalme wa giza wa Shetani siyo mageni. Yanaonyesha dhahiri jitihada za Shetani kwa miaka kupingana na Ufalme wa Mungu. Anatoa mbadala wa kile ambacho Mungu anatimiliza kwa kupitia nguvu za Roho Mtakatifu.
Twasoma katika kitabu cha Kutoka juu ya nguvu ya walozi wa Misri waliojaribu kufanya miujiza Mungu aliyofanya kwa mkono wa Musa. Na kwenye kitabu cha Ayubu, Shetani anadhihirishwa kama mwenye wivu sana juu ya uaminifu wa Ayubu kwake Mungu. Alitumia ukatili na unyang’anyi ili ajaribu kumlazimisha Ayubu kwenda kinyume na Mungu.
Njia za shetani zinatambuliwa na: Woga, vitisho, ahadi za kupata anasa na nguvu, misukumo, mashaka, na tuhuma. Baadhi ya mambo ya kwanza anayoyatambulisha kwetu yanaonekana ni ya kuvutia sana na ya kusisimua. Anashauri, “Ungependa kujua mambo ya mbeleni au kuwa na ufahamu ambao wengine hawawezi kuwa nao?” Anaweza kukupa uponyaji ambao uko nje ya idara ya kisayansi. Utabiri wa mambo yajayo huenda unaonekana kwamba hauna madhara wala ubaya, lakini unafuatwa na mengine ya uchawi wa macho, pamoja na kutumia dawa za kienyeji na uchawi wa kumroga mtu, na hatimaye kumpelekea mautini. Wazo linaanza kutuingilia kuwa kuna baadhi ya roho za kuheshimiwa na kuogopwa kwa sababu ya nguvu zilizo nazo juu yetu. Kwa hiyo, Shetani anawanasa hao wasiokuwa waangalifu kwenye mtego wake wa kuendeshwa na woga kwake na roho zake.
Watu wengi sana wamekamatwa na shauku ya vitu ambavyo, kwa mara ya kwanza vilionekana kuwa vyema. Kwa kufanya majaribio ya utabiri wa mambo yajayo na uchawi wa aina mbalimbali, watu wanajiweka kwenye mazingira hatarishi ya kusumbuliwa zaidi na mapepo ya giza.
Lengo la shetani ni kumomonyoa na hatimaye kuharibu imani ya mkristo kwa Mungu. Mkristo apata ushindi kwa kuwa na imani kwa Yesu Kristo peke yake. Wakati mwingine hamu ya kujua visivyojulikana au matamanio ya nguvu vinamsukuma mtu afanye majaribio na hayo ambayo ni ya ufalme wa Shetani. Imani ya kukaza kwa Mungu humpumzisha mtu asivutiwe na yale yasiyojulikana na pia inamimarisha kabisa katika nguvu za Kristo.
Yale yaliyoanza kutokana na shauku au majaribio punde yanamnasa mtu kwenye wavu wa hofu, hofu ya kile kinachoweza kutokea mbeleni, hofu ya nguvu kuu, hofu ya watu wengine, hofu ya Shetani mwenyewe. Hizi hofu zinamfunga mtu aliyeruhusu mwenyewe kujihusisha na matendo yasiyo na uhakika. Kutibu hofu hii, Shetani anadai kuwa anao dawa nzuri: Eti atatoa nguvu zaidi kama mtu atajisalimishia utaratibu fulani au kutii amri kadhaa. Shetani asema kwamba hofu ya roho nyingine zinaweza zikashindwa kwa kujipatia nguvu kubwa zaidi kwetu wenyewe. Kwa hiyo mtu anaingizwa kwenye hatua za kufikia nguvu zaidi ambazo, badala ya kumpandisha kwenye kiwango cha juu cha amani, zinamzamisha chini katika kina kirefu cha machukizo ya kishetani. Usalama ulioahidiwa na shetani hauonekani, na hubadilishwa kwa uhitaji wa kulindwa na nguvu zilizo juu zaidi kwenye huu ufalme wa uovu. Huu ndio mfumo wa kishetani.
Mpango wa shetani ni kumzidi Mungu. Shetani aliumbwa kuabudu, na sio kuabudiwa. Yeye sio nguvu ya juu; hawezi kumzidi Mwana Kondoo wa Mungu; hawezi kutoa amani; hana nia na ushindi wetu. Hata hivyo anaendelea na kazi ya kuwatawala watu ili watu wamtumikie yeye. Anajaribu kuleta mashaka kuhusu Mungu na ufalme wake. Anajitahidi kuanzisha taasisi yake na yeye akiwa kama mfalme. Hii inaendelezwa kwa utaratibu wa hofu na udanganyifu wa nguvu. Anafanya miujiza ili awashangaze na kushawishi watu kusudi awawekee kifungo akilini mwao (2Wakorintho 11:14,15). Madhara ya mtego huu ni kuharibu amani na usalama kwa watu binafsi, majumbani, na hata serikalini. Hio inawakamata watu, na inasababisha wajisikie kutishwa sana kama watajaribu kutorokea ufalme huo.
Shetani ni mkali sana, mchoyo sana, mkatili sana, adui mbaya sana uliye naye wewe. Yeye hana heshima hata kidogo. Yeye ni mwongo. Hakuna ukweli ndani yake- “Yeye ni mwongo, na ni baba wa huo ” (Yohana 8:44). Yeye ni muuaji, mharibifu. Yeye ni mfano wa chuki na uovu. Yeye ni mwovu kabisa ambaye hana uzuri uliobakia kwake!
Shetani ni mchochezi wa maovu yote. Hakuna kosa wala dhambi ambayo kwake ni ovu sana au chafu sana kwake. Yeye ni chanzo cha chuki zote, mauaji yote, kila aina ya kutesa watoto au kupiga wanawake, kila aina ya madawa ya kulevya, kila aina ya uzinzi, ndoa zote zilizovunjika, kila aina ya kutokuelewana, kila uchawi, kila kutokuwa na uaminifu. Anafurahi kusababisha hamu ya kuvunja sheria na uovu, uvunjaji wa sheria unaofanyika juu ya watu wengine wema ambao, kwa bahati mbaya, wanaangukia mikononi mwa wasio haki na wapotovu. Yeye ni mkatili na hana msamaha. Hana huruma kwa hao wanaopata mateso. Kumwaga damu na vifo ndio silaha anazotumia kutekeleza kazi zake. Amekuja “kuiba, kuua, na kuharibu” (Yohana 10:10).
Mwisho wa milele wa Shetani ulishaamulika. Kuna sehemu ya moto wa milele ilishaandaliwa kwa ajili yake na malaika wake (Mathayo 25:41). Anajishughulisha na kupata watu wengi kadiri atakavyoweza ili wapate hayo mateso pamoja naye. Anajua anaweza kufanya hivi kwa kuimomonyosha, kuidhoofisha, na mwishowe kuiangamiza imani yetu kwa Mungu. Atafanya hivi kwa kulipinga Neno la Mungu kwa uwazi, ama kwa ujanja na werevu anawahamasisha “wakristo” walio vugu vugu, wasiojali, na waliokubali Ukristo usio na masharti.
Kuna ukombozi kutoka kwenye umiliki na utumwa wa Shetani. Atakufanya uamini ya kuwa hakuna njia ya kutoka. Biblia inatuambia ya kwamba Yesu alikuja kuwaweka huru waliotekwa mateka. Amekuja kuleta uzima. Yesu ni njia, kweli, na uzima (Yohana 14:6). Wakati alipokuwa hapa duniani, Yesu alionyesha nguvu zake juu ya Shetani kwa kushindana na majaribu ya Shetani na akitupa nje nguvu za giza kwa kutumia Neno la Mungu (Mathayo 4:1-11; Marko 9:25,26). Yesu alishinda nguvu za Shetani kwa kifo chake msalabani na kufufuka kwake kutoka wafu.
Je, tunawezaje kujumuishwa katika ushindi huo wa kumzidi huyu adui mkuu wa nafsi zetu? Kwanza, lazima tufahamu ya kwamba tulikuwa tumetekwa na shetani na kufungwa na hofu yake. Lazima tukubali kwamba huku ni hali ya dhambi na kwamba tumepotea tukibakia hali hii. Tunapogundua hili kwamba hatuwezi kujiokoa wenyewe kutoka mkononi mwa Shetani, lazima tumlilie Mungu ukombozi wake kwa moyo wetu wote. Lazima tuzitubu na kuziacha dhambi zetu. Twahitaji kukubali kwa imani, damu ya Yesu Kristo yenye utakaso kwa ajili ya dhambi zetu. Lazima tujitoe nafsi zetu kwa Mungu, kukubali msamaha wake na kwa uaminifu kutii Neno lake. Tunapotimiza haya masharti, anatupa amani kwake, anayatuliza mahangaiko mioyoni mwetu, anasamehe dhambi zetu, anatufanya kuwa kiumbe kipya na kutufanya mmoja wa wanawe. Hii ndio inamaanisha kuzaliwa upya. Yeyote anayepinga mwito wa Mungu bado yumo katika ufalme wa Shetani, na mwishowe, mdanganyi atampeleka huyo mtu pamoja naye kwenye mateso ya milele.
Kama huelewi mpango ambao Mungu amekuwekea, jifunze Neno la Mungu, na umwombe Yeye kwa uaminifu moyoni, na atakuonyesha njia. Mungu anakuita kwake na anataka wewe utoroke na utumwa wa Shetani. Mungu akubariki. Soma Zaburi 91.
Masomo Mengine:
Luka 11:20-23 Mmoja mwenye nguvu zaidi ya Shetani
Warumi 6:20-23 Kuwa huru kutoka kwenye dhambi
Isaya 61:1 Kuwekwa huru mateka
Warumi 8:1,2 Kuwa huru na laana na hatia