“Tazama wapendezwa na kweli iliyo moyoni” (Zaburi 51:6).
Uaminifu ni maadili ya ukweli katika kufungamana na mambo yote ya maisha. Kwa hakika uaminifu ni jambo la moyoni, pia ni fundisho la msingi la Injili ya Yesu Kristo. Mungu anajua mawazo na makusudi ya moyo. Anatambua ukweli kama msingi muhimu kwa maana yeye ni Mungu wa ukweli. (Kumb. 32:4) Hakika atabariki uaminifu uliokamilika wa moyo wetu.
Je, unao tabia ya kusema ukweli wakati ungeweza kupatikana na jambo, lakini ukawa si mwaminifu wakati ambao hakuna atakayekugundua?
Je, kwa makusudi unaweza kumridhisha mtu kwa ushawishi usio wa kweli?
Je, unaweza kufanya manunuzi kwa kukopa wakati ulifahamu kwamba huna uwezo wa kulipa?
Je, unamwambia Mungu jinsi mambo yalivyo wakati unapomwomba?
Je, kwa uaminifu unalitenda kila jambo ambalo unafahamu Mungu anakutaka ulitende?
Je, wewe ni mwaminifu kuhusu mafundisho ya Biblia?
Je, jinsi unavyojifanya kuonekana, kweli ndivyo ulivyo?
Kuna hadithi ya kuchochea hisia katika Agano Jipya ya mtu aitwaye Anania na mkewe Safira katika kitabu cha Matendo 5:1-11. Waliuza mali yao kama wengine nao walivyofanya na kujifanya kutoa fungu lote kwa kanisa, wakati kwa hila walikubaliana kubakiza sehemu ya malipo kwa ajili yao. Anania na Safira walileta pesa hizi mbele ya viongozi wa kanisa wakisema kwamba waliuza shamba hilo kwa kiasi hicho walicholeta. Udanganyifu wao ulihukumiwa na Mungu mara moja na kuadhibishwa kwa kifo. Katika habari hii ya kanisa la mwanzo, unafiki (au udanganyifu) ulikuwa ukiadhibishwa kwa ukali. Mungu hapuuzi uzushi huu. Nasi kama Anania na Safira huenda tunaweza tukatoa uzushi unaoridhisha hata kama maneno tuyasemayo siyo ya uongo. Twaelekea kusahau uwajibikaji wetu mbele za Mungu. Mungu ajua jinsi mioyo yetu ilivyo, na anatutegemea tuwe waaminifu na wa kwelikweli.
Mnafiki hujifanya kuwa mtu ambaye siye yeye. Huenda anadai kuwa mwaminifu, lakini wakati ambao ingekuwa manufaa kwake, yuko tayari kusema uongo. Labda anaweza kuzungumzia vizuri kuhusu mahitaji ya wasiobahatika, lakini siye mkarimu wa kutoa muda wala msaada wakati maafa au matatizo yakitokea. Mtu mwingine aweza kujifanya kuwa mkarimu kujishughulisha na mambo ya majirani zake, na bado akatumia fursa hio kuwasengenya. Mwingine huenda anajionyesha kuwa mtu mnyofu, lakini bado yuko tayari kuchukua pesa za mtu mwingine, maadamu asigunduliwe katika tendo hilo. Huenda atajaribu kujiaminisha binafsi kwamba anaishi maisha ya juu kitabia kuliko watu wengine wakati yeye ni mdanganyifu. Mtu aliye na tabia hizi ni mnafiki wala si mwaminifu.
Unafiki wa wanadamu kila wakati ni kitu cha kumhuzunisha Mungu. Yesu asema, “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami” (Mathayo 15:8). Changamoto kubwa kwa mwanadamu ni kuweka mdomo na moyo kwa pamoja. Uaminifu kutoka ndani yetu ndio ufunguo wa kupata neema na fadhili kwa Bwana.
Mkristo wa kweli ni mfano wa uaminifu. Kustawi kwake kiroho huendana na unyofu wake mbele ya Mungu. Uaminifu kwa binadamu wenzetu pia ni muhimu na unahitaji usikivu wa umakini. Katika maneno yetu, matendo ya shughuli zetu, na hata makubaliano ya kibiashara ni lazima tuhifadhi imani kwa watu wote. Ili tutende hili, ni lazima tuwe tayari kupata hasara kwa ajili ya ukweli.
Kuna somo tunaloweza kujifunza kutokana na simulizi hii. Mwalimu alimwuliza kijana mmoja swali:
“Je, ungesema uongo ukilipwa shilingi 50?”
“La hasha, mama” kijana akamjibu.
“Je, ungeweza kusema uongo ukilipwa shilingi elfu mbili?”
“La hasha, mama” kijana akamjibu.
“Je, ungeweza kusema uongo ukilipwa shilingi milioni mbili?”
“Lo!” akajisemea moyoni. “Ni kitu gani nisichoweza kukifanya nikiwa na shilingi milioni mbili?”
Wakati akisitasita, kijana mwingine nyuma yake akasema, “La hasha, mama”.
“Ni kwa nini?” mwalimu akauliza.
“Kwa sababu uongo unashikamana na mtu. Wakati hio hela zitakapoisha, na vitu vyote vizuri vilivyonunuliwa na pesa hizo vimetoweka, UONGO utabakia pale pale ulipo.”
Ukweli una umuhimu kiasi kwamba tungekuwa tayari kusumbukiwa kwa ajili yake. Sisi tukiwa tayari kusema uongo ili tujiokoe kutoka kwa kuaibishwa kwa muda mfupi, ni gharama kubwa mno kulipa kwa ajili ya kupotewa na uadilifu wetu. Pesa zipatikanazo kwa njia ya ujanja ni malipo duni kwa kujipatia dhamiri iliyonajisika, na hukumu ya milele ya Mungu inayokuja.
Je, wasema kwamba unatembea katika nuru ya Mungu na wakati huo huo unayatenda matendo maovu kama:
- Unakataa kumsamehe ndugu au dada yako?
- Hufanyi mapatano unapomtendea mtu vibaya?
- Unatia chumvi kwenye ukweli?
- Unavunja ahadi zako?
- Unamwibia Mungu sadaka na zaka zake?
Uaminifu ni mtihani wa moyo. Mungu anafahamu mioyo yetu, na hakuna kitu kilichositirika kwake. Walakini wakati mwingine hatuwezi kumwambia Mungu kwa kadiri anavyotujua na jinsi tunavyojihisi ndani mwetu. Huenda hatuwaonyeshi jinsi ndivyo tulivyo kwa watu wengine. Mtu wa kweli mwenye furaha ni yule aliye mwaminifu mbele za Mungu, na anajikubali na kukiri jinsi alivyo. Na tukifungua mioyo na maisha yetu kwa Mungu, matatizo haya yote yanatatuliwa.
Malengo na misimamo yetu yanahitaji kuwasilishwa kwenye kipimo cha uaminifu. Kufaulu mtihani huu katika matendo yetu kwa Mungu na wanadamu, twahitaji mabadiliko ya ndani ya moyo, kwa maana mambo ya nje yanafafanua utu wetu wa ndani. Je, wewe ni mwaminifu? Mungu anatudai unyofu, watu wengine wote wanautegemea, na sisi wenyewe tutanufaika kwa kuushika. Ndiyo maisha yaliyo na thamani. “Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia.” (Waebrania 13:18 Tafsiri la NENO). Soma pia Mambo ya Walawi 19:35-36 na Mithali 19:5.