Hili ni swali zuri sana ambalo kila mmoja anapaswa kujiuliza. Biblia inaongelea njia kuu mbili tu; njia ya kwenda Mbinguni na njia ya kwenda Jehanamu. Mbinguni ni sehemu yenye kila kitu kizuri, na ni makao ya Mungu. Jehanamu ni mahali pa dhambi na maharibifu yasiyo na mwisho. Ni sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya Shetani na watoto wake. Je,nifanye nini ili niweze kufika mahali ambapo ni nyumbani mwa Mungu? Kama wewe si mkristo sahihi, na haujazaliwa kwa mara ya pili, basi unahitaji wokovu.
Maana ya kuokoka au kuzaliwa upya ni nini? Inamaanisha kupewa moyo mpya ambao unapenda kufanya yale Mungu aliyoyasema (Ezekieli 36:24-27). Inamaanisha kuacha yale matendo na maneno yote maovu pamoja na mawazo yetu maovu, na kumruhusu Yesu atuonyeshe yale tunayopaswa kuyafanya ili tumpendeze. Ina maana tumruhusu Yesu atuoshee dhambi zetu zote na kufanya mioyo yetu kuwa safi ili isiwepo dhambi itakayotutenga na Mungu(Matendo 3:19). Inamaanisha kubadilishwa kuwa mtu mpya ambaye hupenda kufanya yale tu yaliyo mema machoni pa Mungu, kama Moses alivyochagua kumfuata Mungu, na kama Mariam alivyopenda kuketi miguuni pa Yesu akisikiliza maneno yake (Waebrania 11:25; Luka 10:42).
Je, ni nani anayepaswa kuokoka? Kila mwanaume na kila mwanamke, kila mvulana na kila msichana ambaye ana umri wa kumwezesha kutambua mema na mabaya, mtu yeyote ambaye amefanya lisilo jema, yaani WOTE wanahitaji kupata wokovu. Isaya alisema, “Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe” (Isaya 53:6). Kila mmoja amefanya maovu ambayo hayampendezi Mungu, na hayo maovu yamefunika uso wetu kiasi kwamba hatuwezi kumwona Mungu (Isaya 59:2). Sasa lazima tufanywe kuwa watu wapya. Yesu aliweka dhahiri sana ukweli huu kwa Nikodemu, ambaye alikuwa mwalimu wa Israeli, Yesu alipomwambia, “Amin, amin , nakuambia, mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3-8). Yesu alimwambia Nikodemu ya kuwa ni kuzaliwa kiroho, na Roho Mtakatifu ndio atafanya hilo litokee. Hatuwezi kuona kitendo hicho kwa macho kama mtoto mdogo anapozaliwa, ila tunaweza kujisikia kikitokea, kama vile tunavyoweza kuhisi upepo kwenye uso wetu.
Yesu anatuambia leo, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:28-30). Dhambi inakuwa kama mzigo mzito kwa mtu, wakati anapofikiri kuhusu kukutana na kifo na hukumu ya makosa yake. Yesu anatusihi tumpelekee kila dhambi tuliyo nayo maishani mwetu, na tuzishushe zote miguuni pake. Yesu anataka “tupokee upatanisho”(Warumi 5:11) na tuwe huru na mizigo yetu mizito. Yesu ameteswa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, na alimwaga damu yake, na alikufa msalabani kama dhabihu “kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote”(1Yohana 2:2). Ni lazima tuwe tayari kuona ya kwamba tumetenda dhambi, na lazima tutambue ya kwamba tuna hatia. Halafu inabidi tuamini ya kuwa Yesu aliteswa na alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, na ametulipia gharama ya dhambi zetu. Kwenye Mithali twasoma, “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa: bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”(Mithali 28:13).
Kuna tumaini kwako hata kama wewe ni mwenye dhambi mkubwa. Bwana anasema, ”Haya njoni tusemezane. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu” (Isaya 1:18). Ijapokuwa dhambi zetu ni nyeusi kama usiku, Yesu anataka kuzisafisha ziwe nyeupe kama nguo mpya. Mungu anatusihi tumwendee na dhambi zetu zote na kuzungumza naye juu ya hizo dhambi. Halafu Yesu anataka kutusafisha hizo dhambi kwenye damu yake, ili tuwe na “wale walioshinda kwenye dhiki kuu na kuosha mavazi yao na kuyafanya meupe kwa damu ya mwanakondoo” (Ufunuo 7:14). Huyo mwanakondoo ni Yesu Kristo ambaye alimwaga damu yake pale msalabani kwa ajili yetu.
Biblia inatuambia ya kwamba kila mmoja wetu, wanaume kwa wanawake, wavulana kwa wasichana, tumekuwa mwenye dhambi na tumepoteza utukufu wa Mungu (Warumi 3:23). Lakini Mungu hatuachi bila tumaini, kwa kuwa Mungu anamuamuru kila mmoja kila mahali atubu (Matendo 17:30). Tukiungama dhambi zetu, Mungu atatusamehe dhambi zetu na atatusafisha njia zetu mbaya (1Yohana 1:9). Ikiwa tumemwudhi ama tumemkosea mtu, ama tukimwibia kitu ama kumdanganya, ama tumesema uongo ama tukifanya kitu kingine chochote ambacho ni dhambi, lazima tuzungumze na huyo tuliyemtendea mabaya, pamoja na Mungu, na kuwaambia hali halisi. Kama tumechukua kitu ambacho si chetu ni lazima tumrudishie au tumlipe gharama yake, au kuweka sawa kwa namna nyingine na yule tuliyemwibia. Luka anatusimulia hadithi ya Zakayo. Zakayo alikuwa tayari kurudisha mara nne ya mali alizochukua ambazo hazikuwa halali yake(Luka 19:1-10). Lazima tuhuzunike moyoni kwa sababu ya dhambi zetu, na tuwe tayari kurekebisha matendo maovu, kama Zakayo alivyofanya. Pia inatupasa kufanya amani na wale tuliowakosea. Hii ndio kumrudia Bwana wetu Yesu kwa moyo wako wote, na roho yako yote, na akili zako zote, na nguvu zako zote (Marko 12:30).
Lazima tuamini mioyoni mwetu kwamba Mungu alimfufua Yesu kwenye mauti, na kwamba Yesu yupo hai leo. Wakati tunaamini hili, basi inabidi tukiri ya kuwa Yesu ni Bwana wetu na Mwokozi. Kama tutaungama dhambi zetu zote na tutamwamini Yesu Kristo na moyo wetu wote na nguvu, na tukimkiri kwa mdomo wetu, basi tutaokolewa (Warumi 10:9). Yesu amesema anasimama mlangoni akibisha hodi. Mtu yeyote akiisikia sauti yake, na kuufungua mlango, ataingia moyoni mwake, na atafanya moyo huo makao yake (Ufunuo 3:20). Yesu anasema atakaa na mtu huyo maadamu huyo mtu yuko tayari kumtii Mungu. Eh ni utamu kiasi gani kujua Yesu! Amechukua dhambi zetu zote, na tunayo “amani iliyokamilika kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” (Warumi 5:1).
Kila mmoja aliyepata msamaha wa dhambi, na amani ya Mungu ni kiumbe kipya kwa sababu hafanyi maovu aliyokuwa anafanya awali. Mambo ya kale yote yamekwisha na anaishi maisha mapya na Mungu. Kila kitu ni kipya kwa sababu Mungu anamwongoza huyo mtu, na Mungu anamwambia jinsi ya kuishi (2Wakorintho 5:17). Hajisikii lawama tena, na habebi mzigo mzito wa dhambi kila wakati kwa maana anatembea na Roho wa Mungu (Warumi 8:1). Mambo ambayo macho yanapenda kutazama, na mwili huu wa duniani unapenda kufanya, na kiburi cha maovu kinachotoka kwa Shetani, na maovu mengine yote tunayosoma katika Wagalatia, HAYAPO kwenye maisha ya mtu huyo tena (Wagalatia 5:19-21; 1Yohana 2:15-17). Yeye ni kiumbe kipya na anafurahia matunda yote ya Roho Mtakatifu ambayo tunayasoma katika Wagalatia. Anajua kuwa anayo ahadi “ya maisha ya sasa, na yale yajayo” (1Timotheo 4:8; Wagalatia 5:22-25). Mtu huyo sasa ni Mkristo mwenye furaha sana aliyeokoka, na anao uhakika ya kwamba yeye ni mtoto wa Mungu.
Baada ya kuzaliwa upya, na kupata amani hii na Mungu, ni lazima uendelee kutembea kwa “ujasiri katika fundisho la Mitume” kama vile Mitume wa Yesu walivyofanya (Matendo 2:42). Ni lazima uwe makini kufanya yale Yesu aliyokuambia kufanya, na usimruhusu Shetani akusukume pembeni ya njia ilionyooka tena. Usimwache Shetani akuibie amani ya Mungu tena. Uwe makini sana Shetani asije akakushawishi kurudia tena yale maovu ambayo yalikuwa ni mzigo mzito uliolemewa nao awali. Ongea na Mungu kila siku, na umwombe Mungu akuongoze njia ya mbinguni ambako hakutakuwa na dhiki wala mateso, bali amani na furaha milele (Ufunuo 21:1-7).