Bwana Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wanadamu kutoka kwa dhambi zao. “Bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa akawa ana mfano wa wanadamu” (Wafilipi 2:7). Alikufa kwa ajili ya dhambi za watu wote ulimwenguni, alizikwa na akafufuka tena (1Wakorintho 15:4), kisha akapaa kwenda mbinguni tena (Matendo 1:9). Mitume walimwona na pia waumini zaidi ya mia tano, baada ya kufufuka. Baada ya kupaa kwenda mbinguni, malaika wawili waliwaambia mitume kwamba kurudi kwake kutafanana na kupaa kwake. Ni Mungu tu ndiye anayefahamu ni lini Bwana atarudi. Huenda itakuwa ni jioni au usiku wa manane, au wakati wa asubuhi au alasiri. (Marko 13:35) “Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja” (Mathayo 24:44).
Baadhi wametabiri wakati wa kurudi kwake, hadi siku na saa. “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila baba peke yake” (Mathayo 24:36). Atakuja haraka kama vile umeme utokavyo mashariki hadi magharibi (Mathayo 24:27). Atakuja wakati tusiotarajia kama mwizi anavyokuja usiku (2Petro 3:10). Siku hio itawajia kwa ghafla, kama mtego unasavyo (Luka 21:34). Bwana, katika hekima isiyo na vikomo, atarudi kumlipa kila mtu sawasawa na alivyotenda (Ufunuo 22:12). “Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, kesheni” (Marko 13:37).
Dalili za Nyakati na za Kurudi Kwake
Bwana ameeleza dalili ambazo kwazo tuweze kutambua kwamba kurudi kwake kumekaribia. “Basi, kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu: Nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa u karibu, milangoni” (Mathayo 24:32-33). Kutakuweko:
- Vita na matetesi ya vita (Mathayo 24:6)
- Taifa litaondoka kupigana na taifa (Mathayo 24:7)
- Matetemeko ya nchi, njaa na tauni (Mathayo 24:7)
- Uovu utaongezeka, upendo utapoa (Mathayo 24:12)
- Makristo na waalimu wa uongo (Mathayo 24:11, 24; Marko 13:22)
- Siku kama wakati wa Nuhu (Mathayo 24:37)
- Ishara katika jua, mwezi na nyota (Luka 21:25)
- Mshangao wa mataifa na msukosuko (Luka 21:25)
- Watu wakivunjika mioyo kwa hofu (Luka 21:26)
- Watu wakisema amani na usalama (1Wathesalonike 5:3)
- Nyakati za hatari (2Timotheo 3:1-5)
- Wapendao anasa na wenye mfano wa utauwa (2Timotheo 3:1-7)
- Watu waovu wakizidi kuwa waovu (2Timotheo 3:13)
- Ukengeufu (Uasi) (2Wathesalonike 2:3)
- Kujiweka akiba kwa ajili ya tamaa za kimwili (Yakobo 5:1-15)
- Wenye kufanya dhihaka (2Petro 3:3-10)
- Watu wenye kudhihaki wafuatao tamaa zao (Yuda 16, 17, 18)
Siku hizi asilimia kubwa ya dalili hizi zimedhihirishwa tayari. Uzinzi, uasherati, kuvunjika kwa ndoa na kuoana na mwingine, ushoga, uhalifu, na maovu yanaongezeka kwa haraka na kutapakaa kwa mapana. Hayo yote na dhambi zingine zinaharakisha kurudi kwa Bwana. Mambo haya yameandikwa “mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu” (2Petro 3:2). Watenda dhambi wataogopa kuona ujio wake, lakini watakatifu wataushangilia.
JE, UKO TAYARI? Unayo amani na Mungu na wanadamu wenzako? Je, kuna jambo lo lote katika maisha yako linalokuzuia kusema, “Amina; na uje, Bwana Yesu” (Ufunuo 22:20)?