Biblia hutuambia kwamba Mungu anajua kila kitu, na kwamba anahifadhi maandishi ya maisha yetu. Tutahitajika kutoa maelezo ya aliyoandika siku ya hukumu (Warumi 14:11-12). “Na niliwaona wafu, wadogo kwa wakubwa wamesimama mbele ya Mungu; na vitabu vilifunguliwa: na kitabu kingine cha uzima kikafunguliwa, na wafu walihukumiwa kwa yale yaliyoandikwa katika vitabu kulingana na kazi zao” (Ufunuo 20:12). Tutakaposimama katika hukumu mbele ya Mungu, tutakuwa tumechelewa kubadili maisha yetu wala mwisho wetu wa milele.
Mungu huona yote, mema na maovu tunayoyafanya. Yeye hufahamu msimamo wetu halisi na mawazo yetu--- ikiwa mema au maovu. “Wala hakuna kiumbe chochote kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote ni utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu” (Waebrania 4:13). Tutahukumiwa kwa orodha ya matendo yetu. “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya” (Mhubiri 12:14).
CHAGUO NI LETU
Katika uhai huu tunaweza kuchagua kumfuata Kristo na mafundisho yake au kufuata tamaa ya mwili wetu unaopenda dhambi. Biblia ina orodha ya dhambi za mwili katika Wagalatia sura ya 5. Ndiyo haya, “Uasherati, uzinzi, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, ugomvi,wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo” (Wagalatia 5: 19-21). Ikiwa baadhi ya haya yamepatikana kwetu, andiko hili hutuambia kwamba hatuwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Kwa neema ya Baba wa Mbinguni aliye na upendo, tukitubu na kumwamini Kristo, tunapata msamaha. Kisha damu ya Kristo hufunika dhambi na zinafutwa kwenye orodha.
Pia Biblia inayo orodha ya matunda yanayozalishwa katika maisha yetu tunapojitoa kwa Mungu. “Lakini matunda ya roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utulivu, wema, imani, upole, kiasi…..” (Wagalatia 5:22-23). Ni muujiza wa neema kuwa na matunda haya pamoja na majina yetu kuandikwa Mbinguni.
Neno la Mungu hutuonya juu ya mtego na hatari ambayo inatukabili. “Pia jueni hili, kwamba katika siku za mwisho nyakati za hatari zitatokea. Kwa maana watu watajipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu, wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao” (2Tim 3:15). Ni dhahiri kwamba hali zilizo katika ulimwengu hazifai maisha ya ukristo. Tumezungukwa na uovu wa kila namna ya ulaghai. Kwa kuwa tunawajibika kwa kila neno na tendo letu, tunapaswa kufanya chaguzi ambazo zitazalisha matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu.
Katika Biblia kuna mafungu mengi yanayotuonya kuhusu kutokujali wokovu wetu. “Na kama wenye haki hawaokolewi, Je, watakuwaje wenye dhambi na wasiomcha Mungu?” (1Petro 4:18). “Na Bwana alimwambia Musa, yeyote anitendaye dhambi, nitafuta jina lake katika kitabu changu” (Kutoka 32:33). “Njooni mmtazame mtu (Yesu) aliyeniambia yote niliyoyatenda” (Yohana 4:29). Ingawa maneno haya ni yenye uzito Mungu ameahidi kutusamehe dhambi kama tumeamini na kutubu katika damu ya Kristo ya kulipia deni. Atazifuta dhambi zetu badala ya kufuta majina yetu kutoka kwenye orodha.
JE, JINA LAKO LIPO KATIKA KITABU CHA UZIMA?
Ili majina yetu yaandikwe katika kitabu cha uzima, ni lazima tuukubali mwaliko wa Yesu: “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao, na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28). Hakuna anayesamehewa hatia ya dhambi pasipo damu ya Yesu. Yeye kwa sababu ya upendo, alimwaga damu yake kwa hiari juu ya msalaba kwa ajili ya dhambi zetu. Yesu alimwambia Nikodemo, “Mtu asipozaliwa kwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3). Pia alisema, “Msipoongoka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni” (Mathayo 18:3). Yesu huwaalika kila mmoja kuja kwake na kuokolewa.
Baada ya majina yetu kuandikwa katika kitabu cha uzima tusitake yafutwe tena. Yesu asema, “Tazama, naja upesi: Shika sana ulicho nacho asije mtu akaitwaa taji yako” (Ufunuo 3:11). Na tena, “Kesheni mkiomba, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo 26:41). Maandiko haya yanatuonya kuwa wanaokesha na siyo kuacha ahadi yetu ya kumtumikia Mungu. Shetani, adui wa nafsi zetu, ameelezwa kama simba angurumae, ambaye ataturarua tusipompinga kwa kuwa imara kwenye imani. (1Petro 5:8-9) Tunapaswa kulichunguza Neno la Mungu na kuwa thabiti katika sala zetu, la sivyo wokovu wetu utatuteleza. Tumeahidiwa, “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, na sitaondoa jina lake katika kitabu cha uzima, lakini nitakiri jina lake mbele ya Baba yangu, na mbele ya malaika zake” (Ufunuo 3:5).
KUWA TAYARI KWA SIKU YA HUKUMU
Leo ndiyo siku ya neema, ni nafasi ya kutengeneza nyumba yetu na kujiandaa kwa siku ya hukumu. Tukifa miili yetu inayokufa itarudi mavumbini. Lakini atakaporudi Yesu kuuhukumu ulimwengu siku ya ufufuo, kila mmoja atapokea mwili usiokufa ambao utakaa milele mbinguni au motoni. Kama kuna doa la dhambi mioyoni mwetu, tumgeukie Yesu LEO aisafishe, kisha twaweza kuwa tayari kuingia mbinguni siku hiyo kuu. “Na hakitaingia mle kilicho najisi, wala afanyaye machukizo, wala mwongo: bali wale walioandikiwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo” (Ufunuo 21:27).