Yesu anasema kwamba milango ya mbinguni imefungwa dhidi yako isipokuwa unazaliwa mara ya pili. Kwa hiyo twauliza: “Rafiki, umezaliwa mara ya pili?” “Muumini wa kanisa, umezaliwa mara ya pili?” Ikiwa hapana, basi umepotea. Kwa maana Yesu anasema, “Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3). Kwa kweli hakuna mtu anayetaka kufa akiwa mwenye dhambi, au kupotea; basi hamna budi kuzaliwa mara ya pili.
Unaweza ukauliza, “Kuzaliwa mara ya pili maana yake ni nini?” Leo, kuna mafundisho mengi ya uongo kuhusu kuzaliwa mara ya pili. Siyo ubatizo, kwa kuwa wengine walibatizwa na bado hawajapata moyo mpya wa kiroho, wala kumpokea Roho Mtakatifu (Matendo 8:9-25). Siyo kujiunga na kanisa, kwa sababu wengine wameingia lakini bado wanatenda dhambi kila siku (Wagalatia 2:4). Siyo kula meza ya Bwana, kwa maana baadhi walikula isiyostahili na iliwaletea hukumu (1Wakorintho 11:29). Siyo kujibadilisha mwenyewe au kujaribu kuishi maisha bora kwa uwezo wako, “kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze” (Luka 13:24). Siyo kusali, kwa maana Yesu asema, “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami” (Mathayo 15:8).
Unaweza kuwazia hivi, “Nikijaribu yote niwezayo: kuwasaidia masikini, kuwatembelea wagonjwa na kuwa mwema kila siku kadiri niwezavyo, basi kwa kweli nimezaliwa mara ya pili.” La, hasha, huwezi kuwa tofauti na jinsi ulivyo moyoni. “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu wala haiwezi kuitii” (Warumi 8:7). “Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.” (Mathayo 7:18) Unapaswa kuwa na moyo uliobadilika. Kwa kuwa Mungu kupitia manabii, asema hivi, “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama” (Ezekieli 36:26).
“Hivyo basi, kuzaliwa upya maana yake nini?” Kiini cha kuzaliwa upya ni kuwa na mabadiliko ya moyo kutoka kwa maisha ya kujitumikia kwa ubinafsi, na kupata maisha ya kumtumikia Bwana. Mabadiliko haya hutokea wakati unapojutia dhambi zako, na kwa imani unamtazamia Yesu kwa kuomba msamaha. Mtoto azaliwapo, uhai mpya unatokea, binadamu mpya katika mwili. Hali kadhalika, unapozaliwa upya kwa roho, uhai mpya huu hutokea ambao ni ndani ya Yesu Kristo na unaongozwa na Roho Mtakatifu. Hivyo basi, kunaitwa kuzaliwa upya. Ni uhai mpya ndani ya Kristo Yesu. “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17).
“Ni lini na kwa njia gani nitegemee kuzaliwa mara ya pili?” Maandiko matakatifu yasema, “Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu....” (Waebrania 3:7-8). Hii inamaanisha kwamba katika umri wowote, wakati wowote, au mahali popote, ukisikia mwito wake na kuitika unaweza kuzaliwa kwa mara ya pili kwa njia ya Roho. Kuzaliwa kwa mara ya pili kunaweza kutokea mara moja unapomtolea Yesu vyote na kumwendea kupata msamaha. Mungu anayechunguza moyo, anaona uaminifu wa moyo wako. Anaumba moyo mpya na kutia roho ya kweli ndani yako. (Zaburi 51:10) Kwa njia hii unazaliwa upya – kiumbe kipya katika Kristo Yesu kwa njia ya kumwaminia. Unapozaliwa upya, Mungu anakufanya uwe mwana na mrithi. “...na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo” (Warumi 8:17).
Hatimaye: “Kwa dalili gani naweza kutambua kwamba nimezaliwa upya tayari?” Paulo katika Warumi 8:1-10 anafundisha; “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo sio wake”. Biblia yafundisha kwamba waliopotea wamekufa dhambini, wamelaaniwa, na wana dhamiri iliyo ya uovu. Wana mawazo yenye tamaa ya kimwili, wasio na tumaini, wasiotii, na wasio na Mungu ulimwenguni. Lakini wewe uliyezaliwa mara ya pili ni mtoto wa Mungu, u hai katika Kristo, umeokolewa, huna hatia ya dhambi, na unayo dhamiri safi. Nawe unayo nia ya kiroho, umejazwa na Roho Mtakatifu na imani, na unalo tumaini la uzima wa milele. Dhambi zako zimeondolewa kwa damu ya Yesu Kristo. Moyo wako umejazwa na upendo na amani wa Mungu zinazozidi ufahamu wote. Unayapenda mapenzi ya Bwana, na unayo shauku na umepewa uwezo kuyafanya mapenzi hayo. Pia unatembea na tumaini la uzima wa milele baada ya kufikia mwisho wa safari yako, na unayo ahadi ya makao yaliyopo mbinguni. Je, mtu anaweza kupata mageuzi kama haya na asiyatambue? La, hasha kwani “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Warumi 8:16).
Ikiwa hujapata mabadiliko haya yaletayo amani na furaha moyoni, usipuuze, mtafute Mungu kwa moyo mmoja. Ni lazima uzaliwe mara ya pili.