Maisha ni magumu. Mateso na magumu ni sehemu ya maisha yetu. Watu wengi kwa wakati mwingine wanaugulia magonjwa ya kimwili. Njaa inawashikia watu kwa asilimia kubwa hapa duniani. Umasikini unawatesa watu wasio na uwezo. Na wengine wapo wanaoteseka mikononi mwa watu kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, baadhi wanashikwa na matatizo ya kindoa, au wazazi wakatili, au mabwana wakali. Kwa sababu ya hali ya vita katika baadhi ya nchi zingine watu wengi wasio na hatia wanapoteza mali, nyumba, familia, na hata maisha yao. Wale wanaomtumikia Mungu kwa uaminifu, wanateswa na kuudhiwa kwa sababu ya imani yao. Ulimwenguni pote watu mamilioni wanateseka kila siku. Kwa nini?
Kuna Sababu Gani?
Mateso yaliingia ulimwenguni tokea mwanzo kwa sababu ya dhambi. Yanawakumbusha wanadamu na hali yao ya kuwa wenye dhambi. (Mwanzo 3:16-19; Warumi 5:12). Kwa sababu Adamu na Hawa waliasi amri ya Mungu katika bustani Edeni, maumivu, mateso, na huzuni yamekuwa sehemu ya maisha ya mwanadamu kila siku. Kwa sababu dhambi iko duniani, mateso ni sehemu ya maisha. Katika maisha haya hapa duniani tusitarajie kuona mwisho wa mateso wala magonjwa kuisha kabisa. Sisi sote tunaathirika nayo bila kujali rika yetu, taifa letu, au cheo chetu.
Watu wengi wanateseka bila lazima kwa sababu wanatumia miili yao vibaya sana, au hawaijali wala kuitunza miili yao. Kama utachagua mwenyewe kuvuta sigara, kunywa pombe, au kutumia madawa ya kulevya, na kuishi maisha bila kujizuia utajiangamiza. Matokeo ya maisha haya maovu ni uharibifu wa mwili wako, na akili yako inaweza kuchanganyikiwa na mawazo mengi ya kukata tamaa. Ni dhambi kuikatili miili yetu (1Wakorintho 3:16-17, 6:18-20).
Utukufu Kwa Mungu Katika Mateso
Kuna mateso mengi ya kawaida yanayotujia sisi sote, tajiri na masikini pia. Hakuna mtu, japo ni mzuri kiasi gani, anayeweza kukwepa mateso yote. Kwa mfano Ayubu, alitambuliwa na Mungu kama mtu mkamilifu na mwenye haki. Angalia misukosuko yake ya machungu: alipoteza afya yake, mali yake yote ikaharibika, watoto wake wakafa wote, na pia mke wake akamgeuka! Badala ya kumlaani Mungu, Ayubu alisema “Bwana alitoa, na Bwana ametwaa: jina la Bwana na libarikiwe.” (Ayubu 1:21). Mungu alitukuzwa kwa sababu imani na sifa za Ayubu. Kadhalika, angependa kutukuzwa tunapopitia mateso yetu.
Mtu aliye mgonjwa, kipofu, mwenye kovu, kiziwi, mlemavu, tasa, n.k. hakupata hali hio kwa sababu yeye au wazazi wake wametenda dhambi. Wanafunzi walimwuliza Yesu baada ya kumwona kipofu: “Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?” (Yohana 9:2) Yesu akajibu, “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake” (mst3). Baadaye Yesu alimponya huyo mtu. Kwa mfano mwingine, mwanamke tasa anateseka bure. Anaachwa na kukataliwa na mume wake kwa sababu ya uzushi na unyanyapaa wa mila na desturi za ukoo. Utasa wake hauonyeshi kwamba amefanya dhambi, wala hajalaaniwa na Mungu. Mwanamke mwenye hali hii, na asikate tamaa kuishi, maana Mungu ndiye anayefunga tumbo, na yeye ndiye anayefungua tumbo. Soma 1 Samweli 1:5; 19-20. Wanawake wenye tatizo hili na waweke imani yao kwa Mungu wakijua kwamba Mungu anawapenda na anawawazia mema na sio mabaya.
Mateso Yana Makusudi Gani?
Mungu hapendi kukutesa; “Maana moyo wake haupendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha” (Maombolezo 3:33), bali anapenda utakaswe kwa kuvumilia mateso ya namna hii. Hata mabadiliko ya kiroho yanaweza kuingia moyoni mwako kwa kupitia mateso hayo. Mateso yanadhihirisha hali halisi ya roho yako jinsi ilivyo na kukuonyesha udhaifu wako. Ukikubali magumu na mateso yanayokujia, yanaweza kulainisha moyo mgumu. Ukiwa mnyenyekevu wa moyo, utamtegemea Mungu na makusudi yake kwa maisha yako. Mungu anakusudia akusogeza karibu naye kupitia mateso yako. Yusufu aliuzwa kama mtumwa na ndugu zake. Badala ya kuwa na uchungu moyoni juu ya hili, alimruhusu Mungu afanye kazi ndani mwake. Mateso ya Yusufu yalikuwa sehemu ya mpango wa Mungu ili familia yake na watu wote wa Misri wapate kuokoka wakati wa njaa. Baadaye aliwaambia ndugu zake waliokuwa wametubu, “Nanyi kweli mlikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo”(Mwanzo 50:20). Alibarikiwa kwa kukubali kwake.
Faraja Ya Mungu Katika Mateso
Mateso unayopitia yanakufanya uifikirie nafsi yako. Unaweza kujiona umebaki peke yako katika matatizo na kufikiri hakuna mtu anayekuelewa. Mizigo unayobeba inaweza kuonekana ni mikubwa kuliko ya watu wote wengine. Ni rahisi kujihurumia na kuwa na uchungu wa moyo, lakini mfano wa Yusufu unakuonyesha ni kwa jinsi gani Mungu aweza kukubariki ukimnyenyekea. Usikate tamaa, bali unaweza kuruhusu mateso yako yabadilishwe yawe ni utukufu kwa Mungu. Wakati utakapompelekea mateso yako yote na kwa unyenyekevu ukinena, “Bwana, mapenzi yako yatimie,” Mungu anaweza kukufariji.
Mateso hayatakuwa na mwisho kwa wale waliomkataa Yesu (Yohana 12:48). Japokuwa, wale walio tayari kuteseka kwa ajili ya Yesu katika maisha yao hapa duniani, watapokea thawabu ya uzima wa milele huko mbinguni ambapo hapana mateso. (Ufunuo 21:4) Kwa kutii na kukubali njia za Mungu kwetu na kuziungama dhambi zetu, mavazi yetu yataoshwa yawe meupe kwenye damu ya Mwana Kondoo. Hao waliokombolewa kwa njia hii watapata taji la utukufu mbinguni. (Ufunuo 7:13-14).
Mateso yanakufundisha kuwahurumia watu wengine wanaoteseka. Ukipitia mateso mwenyewe utakuwa tayari kabisa kuwatembelea na kuwaombea wenye mateso na dhiki. “Atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu” (2 Wakorintho 1:4).
Yesu Ndiye Mfano Wetu
Yesu aliyekwisha kuishi kwenye hii dunia akiwa na mwili huu kama wetu, anatuelewa vizuri pamoja na mateso yetu. Anasononeka nasi zaidi ya mwanadamu mwenzetu yeyote. Anajua maumivu yetu na mioyo yetu yenye kufadhaika. Wakati Yesu alipoona huzuni ya marafiki zake kwenye kifo cha Lazaro, aliguswa sana rohoni mwake na kufadhaika moyoni hadi akalia machozi (Yohana 11:33-35). Yesu alijitoa kuteseka kwa ukombozi wa milele wa mwanadamu. Ikiwa Mwana wa Mungu Mkamilifu alikuwa tayari kuyapitia mateso namna hii, basi inatubidi sisi pia tuwe tayari kuvumilia mateso. Wafuasi wa kweli wa Mungu wanakubali magumu na mateso yanayowajia, kwa sababu wanamtumikia Yesu, ambaye ni mfano wao. Wakiwa na uelewa wa upendo wa Yesu na jinsi alivyojitoa kuwa dhabihu, inawafanya wajiulize, “Kwa nini nasi tusingeteseke?”
Ijapokuwa unaweza kuteseka sana, unaweza kupata utulivu moyoni kwa kukubali yale Mungu aliyoruhusu kwako. Mungu aliye Mpangaji Mkuu, amekupangia maisha yako. Pia amekuahidi kwamba atakulinda katika kila jaribu litakalokuja kwako. Wakati Mtume Paulo alipokubali mateso yake, aliweza kuwa na furaha kama mtu aliyetumikwa. Aliomba mara tatu, akimwomba Mungu aondoe ule mwiba uliomo mwilini wake, lakini Mungu akamjibu, “Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu” (2Wakorintho 12:9). Kuna matukio mengi ambayo watu humshukuru Mungu kwayo yanayowapitisha kwenye bonde la mateso. Maana yaliwafanya wasimame, wajipime, na kuwaza sana juu ya maisha yao. Baadaye wakagundua ya kwamba maisha ni zaidi ya anasa, malengo ya dunia, na kujikidhi haja zao. Wengi wameshuhudia ya kwamba wamempata Bwana kwa kupitia mateso. Halafu wakati watakapokabili mauti ya kimwili, watasema kwa furaha pamoja na Paulo, ”Mauti imemezwa kwa ushindi. Uchungu wa mauti ni dhambi; na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo” (1Wakorintho 15:54, 56-57).
Kadhalika ukijitoa kabisa kwa Mungu na kukubali mateso yako, nguvu ya Mungu itakuwezesha kuyashinda yote. Ukiwa na roho ya kukubali mateso yako na mpango wa Mungu kwa ajili yako, utaweza bado kumshukuru Mungu. Ukiwa na msimamo huu, utabarakiwa kwako na pia utakuwa mshahidi kwa wengine.