Amani, amani iko wapi—kwa mataifa, nyumbani kwetu, na zaidi ya yote kwa mioyo yetu? Kilio hiki kikuu kimesikika kwa vizazi. Je, ni kilio cha moyo wako pia?
Watu wamechoka na kuhangaika. Bila shaka kuna haja ya mwongozo na ushauri, usalama na kujiamini. Tunahitaji na kutaka akili yenye utulivu.
Akili yenye utulivu—Ni hazina iliyoje! Je, hazina hii inaweza kupatikana katika ulimwengu wenye mizozo na kukata tamaa, wenye misukosuko na matata?
Utafutaji mkuu unaendelea! Watu wengi wanatafuta amani katika umaarufu na bahati, katika raha na uwezo, katika elimu na maarifa, katika mahusiano ya kibinadamu na ndoa. Wanatamani kujaza vichwa vyao maarifa na pochi zao utajiri, lakini roho zao zinabaki tupu. Wengine wanakwepa uhalisia wa maisha kwa kutumia dawa za kulevya na vilevi, lakini amani wanayoitafuta huwakwepa. Bado ni watupu na wapweke, bado wapo katika ulimwengu wenye misukosuko na wenye akili isiyo na utulivu.
Mwanadamu katika misukosuko
Mungu alimuumba mwanadamu na akamwekea bustani nzuri apate amani kamili, na furaha. Lakini baada ya Adamu na Eva kutokutii, wakaingia hatiani. Kabla ya hapo walitamani uwepo wa Mungu, sasa wakajificha kwa aibu. Hatia na woga vilichukua nafasi ya amani na furaha walivyokuwa wakifurahia. Dhambi ya mwanadamu ndiyo ilikuwa mwanzo wa ulimwengu usiotulia na akili isiyotulia.
Ijapokuwa roho yetu hutamani Mungu, ubinadamu wetu huasi njia zake. Mapambano haya ya ndani husababisha mvutano na dhiki. Tumehangaika na tunayo wasiwasi. Kadiri tunavyojizingatia sisi wenyewe, ndivyo tunavyozidi kuwa na akili isiyotulia. Mashaka ya maisha na dunia inayobadilika na inayoharibika, hutikisa usalama wetu na kusumbua amani yetu.
Ingawa huenda hujatambua au hujaikabili, dhambi inaweza kuwa sababu ya mashaka yako. Watu wengi hutafuta mambo ya nje na ya kidunia kupata amani. Wanalaumu ulimwengu usiotulia kwa akili yao isiyotulia lakini wanakosa kuangalia ndani ya moyo wao wenyewe.
Yesu Kristo, Mkuu wa Amani
Amani haiwezi kuwepo mpaka nyanja zote za maisha kukubaliana na Yule ambaye anatufahamu sisi. Hili linawezakana tu, tunapokabidhi maisha yetu kabisa kwa Kristo. Yeye siye tu Mkuu wa dunia bali anayajua maisha yetu kuanzia mwanzo hadi mwisho. Alikuwa akitufikiria sisi alipokuja duniani “kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya imani” (Luka 1:79).
Yesu hutoa nuru kwa giza, amani kwa ugomvi, furaha kwa huzuni, tumani kwa kukata tamaa, na uzima baada ya mauti. Yeye husema katika Yohana 14:27, “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa... Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”
Toba Huleta Akili Yenye Utulivu
Ukijihisi umelemewa na mzigo wa dhambi jibu lako ni “Tubuni… mrejee, ili dhambi zenu zifutwe” Matendo 3:19. Yesu huwakaribisha kwa tukio hili lenye maana na la kubadilisha maisha. “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” (Mathayo 11:28). 1 Yohana 1:9 huahidi, “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” Je, utakubali mwaliko wake?
Utakapomjia Yesu, utapata msamaha na uhuru. Badala ya kinyongo na kutosamehe, moyo wako umejawa na upendo na rehema, Yesu akitawala moyoni mwako, utawapenda adui zako. Haya yanawezakana kupitia uwezo wa damu yake Kristo ya kukomboa.
Amani ya kudumu
Kwa Mkristo, imani katika Mungu na kuamini kwamba anatujali, ndilo jibu kwa hofu na mahangaiko. Ni amani iliyoje kumtumaini Mungu asiyebadilika na wa milele hata milele! Yeye anatupenda na atatujali siku zote. Hivyo basi kwa nini tuwe na wasiwasi na kuhangaika. Jifunze kufanya kama tunavyosoma katika 1 Petro 5:7, “Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” Tunayo ahadi, “Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. (Isaya 26:3).
Ukiwa na Yesu Kristo moyoni mwako, utafutaji wako wa amani umekwisha. Yeye atatoa amani na utulivu vitokeavyo tu tunapomtumaini. Utaweza kusema naye mshairi:
Najua amani, ambapo hakuna usalama,
Utulivu, ambapo upepo huvuma,
Mahali pa siri ambapo ana kwa ana
Pamoja na Bwana naweza kwenda.
-Ralph Spaulding Cushman
Utakuwa na akili yenye utulivu katika ulimwengu wenye misukosuko! Fungua mlango wa moyo wako kwa Kristo—sasa hivi tu—na siku moja yeye atakufungulia mlango wa Mbinguni, ambapo amani kamilifu itatawala daima.