Kama inavyotumika katika kitabu hiki, “moyo wa binadamu” humaanisha kikalio cha mapenzi yetu, au “wewe halisi”. Mungu hamtazami binadamu kwa nje, bali hutazama ndani ya moyo wake. Hakuna kilichofichika kwa Mungu.
Moyo ni chemchemi au shina la matendo yote utendayo. Kama moyo ni safi, matendo yatakuwa mema. Kama moyo ni mbovu, matendo yatakuwa maovu. Huwezi kubadili matendo yako ikiwa hujabadilishwa moyoni. “…Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake… Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, hunena yale yaujazayo moyo wake.” (Luka 6:43-45).
Leo kuna watu wengi wenye mioyo iliyofadhaika. Mungu ndiye jibu; anakupenda na anataka kuishi moyoni mwako.
Moyo wa Mwenye Dhambi
Mfalme wa moyo huu ni Shetani; yeye hutawala mwenye dhambi kwa roho zake za uovu. Wanyama waliomo wanawakilisha baadhi ya roho mbaya zinazokaa ndani ya moyo wa mwenye dhambi. Dhambi ni fikira, tendo, au imani yoyote iliyo kinyume na matakwa ya Mungu. Yote haya yanajisi moyo wa binadamu.
Nyoka ni mfano wa: Uongo. Moyo huu hupendi kukabili ukweli, kwa hiyo unaukwepa kwa kudanganya. Unahesabia makosa yake kuwa sawa kwa visingizio.
Mamba ni mfano wa: Tamaa, wivu, na wizi. Nayo huinua kichwa chake kibaya, ikitazama mali ya wengine na kuzitamani. Tamaa inahangaisha mwenye nayo kutafuta pesa kwa nguvu-- hata kwa njia zisizo halali.
Simba ni mfano wa: Hasira na chuki. Mara nyingi hizi hujitokeza kwa kulipiza kisasi na kufoka. Moyo unaweza kuzuia roho yake mbaya kwa muda, lakini baadaye utatapika ukatili wake na ghadhabu kali. Matokeo yake ni kuleta huzuni, maumivu, au hata kifo kwa wenzake na yeye mwenyewe pia.
Mbwa ni mfano wa: Uasherati na uzinzi. Hizi zinakaa hapa pia kwa matendo na mawazo. Yesu alisema kwamba, hata kwa kumtazama mwanamke kwa kumtamani ni kuzini naye moyoni (Mathayo 5:28). Vitabu vyenye aibu, sinema, na ukumbi wa muziki huchochea tamaa za moyo huu.
Nguruwe ni mfano wa: Ulevi, ulafi, na uchafu. Moyo huu hauna kiasi, na huzidisha vitu vyote. Ulevi ni dhambi inayoleta aibu na kuzalisha dhambi nyingine. Ulafi ulihukumiwa kwenye torati kama dhambi mbaya sana (Kumbukumbu 21:18-21). Pengine moyo unaweza kujazwa na maongezi machafu na malalamiko (Mithali 23:29-33).
Buibui ni mfano wa: Kuvuta sigara na matumizi ya madawa ya kulevya. Watu wanaonja maovu haya wakifikiri wataweza kuyaacha, kumbe wananaswa kwenye mtego kama buibui akamatavyo vidudu kwa kujenga wavu wake. Ni sumu zinazonajisi mwili ambao Mungu angependa kutumia kama hekalu lake (1 Wakorintho 3:16-17).
Kobe ni mfano wa: Uzembe, kukawia, na kuchelewa. Pepo hio inamfanya mtu asogeze muda wa kushughulikia dhambi zake , ili asiziache kwa sasa. Akiwa goigoi wa kutokufanya kazi kwa mikono yake, anabaki kuombaomba msaada (Methali 21:25,26). Uvivu wa mwili wake huleta usingizi wa kiroho.
Popo ni mfano wa: Hofu na Uchawi. Unafanyika hasa usiku kama popo atokavyo usiku. Hofu ndiyo inamuendesha mtu kujihusisha na dhambi hizo za siri.
Mungu anachukia mivutio ya kishetani (Isaya 47:12-15).
Tausi ni mfano wa: Majivuno. Hutambulika kwenye moyo huu katika njia zake za maringo na ubinafsi; haujali sana maisha na hisia za wenzake. Unajikweza kwa elimu na mali yake, mitindo ya mavazi, na urembo. Unatamani kupata nguvu, cheo, na heshima. “Kiburi hutangulia maangamizi, na roho yenye majivuno itaangushwa” (Methali 16:18).
Dhamiri huendelea kusumbua moyo hata kama ichomwe kwa chuma cha moto (1 Tim 4:2), hali unabakia katika woga na lawama. Ndivyo Mungu anavyomkumbusha binadamu kwamba hukumu inamsubiri “kwa kuwa roho inayofanya dhambi ndiyo itakufa” (Ezekieli 18:4). Moyo huu hauna amani; ni fujo na vurugu tupu. Ewe moyo unaosumbuka, Mungu anakuita!
Kuchomwa Moyo na Kutubu
Moyo huu wa mwenye dhambi huanza kuitikia mwito wa Mungu. Majuto na huzuni huenea ndani yake ukijitambua wenyewe kama moyo mpotevu. Unafahamu hana lolote la kutuliza hasira ya Mungu inayomsubiri. Unaanza kugundua upumbavu wake ni kama jeraha yenye harufu mbaya na zilizooza mbele za Mungu (Zaburi 38:5). Roho Mtakatifu anamkaribisha mwenye dhambi amtazame Yesu ili apate wokovu. Anamtia mwenye dhambi matumaini.
Mwenye dhambi ameanza kuomba ; mara nyingi siyo kwa mdomo tu lakini kwa kilio cha kukata tamaa ndani ya moyo wake. Anaomba msaada kama mlinzi wa gereza katika Matendo ya Mitume 16:30, “Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?” Anapotambua uovu wa moyo wake analia, “Mungu, nirehemu mimi mwenye dhambi” (Luka 18:13). Sala zake zimepanda hata Kiti cha Rehema. Mungu wa mbingu na dunia ameshaiona hali hii; anasikiliza, naye anaitikia kilio hiki cha kuomba msaada (Kutoka 3:7).
Neno la Mungu linahukumu dhambi na kutoa suluhisho. Linakuja kama mwanga likipenya moyo uliotiwa giza. Kwa neema kutoka kwa Mungu Muumbaji, moyo unapata mwanga na uelewa – mwanga wa kuona dhambi zake zikiangazwa na Maandiko Matakatifu, na uelewa wa kulipokea Neno la Mungu na kulikubali kwa imani. Kazi ya mwenye dhambi sasa ni kuziungama dhambi hizo pasipo kuficha hata moja. Akiweza kufanya hivyo, atakuwa amefungua madirisha yote ya moyo wake na mwangaza mwingi utaingia ndani.
Ujio wa mwangaza wa Neno lenye ukali na nguvu humfukuza nje Shetani pamoja na pepo zake za uovu. Wanapokimbia, Shetani na pepo zake waovu wanapinga mamlaka ya Roho Mtakatifu. Wanajaribu kujificha kwa kufunika dhambi nyingi moyoni kutoka kwenye macho ya uchunguzi wa Mungu.
Moyo huu unapojitoa na kukubali mwaliko wa Yesu, mara anautazama Msalaba…. ulio mahali pa upweke na aibu lakini unang’aa katika rehema zake. Amtazama Mwana wa Mungu ambaye ametundikwa, amejeruhiwa na kutokwa damu. Amevuliwa nguo, kutukanwa, na kuinuliwa juu kwa wanadamu wamuone. Ingawa hana dhambi na ni msafi kabisa, lakini amening’inia katikati ya wezi. “Alihesabiwa pamoja na wavunjaji wa sheria” (Isaya 53:12). Mwenye dhambi anayeumia husikia maneno haya kutoka msalabani, “Baba, wasamehe, kwa kuwa hawajui wanalolitenda” (Luka 23:34). Moyo unaotubu unaanza kulia kwa kusema, “Sioni kosa alilo nalo mtu huyu! Ni dhambi yangu, moyo wangu duni unaostahili kifo cha aibu msalabani na maangamizi ya milele. Ni jinsi gani imewezekana Yesu amechukua adhabu yangu?”
“Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya makosa yetu, alichubuliwa kwa sababu ya uovu wetu; adhabu ya imani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5). Roho Mtakatifu hutunong’onezea hivi, “Dhambi zako zimehukumiwa kwa mateso na kifo cha Mwana wa pekee wa Mungu.” “Lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangilia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu” (Isaya 66:2) ndiyo faraja inayotolewa, kwa moyo unaosikitika chini ya Msalaba.
Nyororo za Shetani zimevunjwa; Roho ya Mungu anaingia sasa akibadilisha moyo huu kabisa. “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama” (Ezekieli 36:26).
Moyo Mpya
Moyo mpya umeumbwa tayari na amani imetolewa na Mungu Baba kutoka Mbinguni. Hali hii ni sawasawa na kuzaliwa upya rohoni. “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.” (2 Wakorintho 5:17). Ukombozi kutoka katika maisha ya dhambi, hadi maisha ya utakatifu umewezeshwa tayari. Dhamiri safi lisilo na kosa huletea moyo huu uhuru. “Sasa hakuna hukumu kwa wale walio katika Kristo Yesu…” (Warumi 8:1). “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” (Yohana 8:36)
Moyo umesulibishwa kwa dunia na njia zake za majivuno (Wagalatia 6:14). Unyenyekevu upo badala yake, kwa maana Bwana wake aliyemfia na kufufuka yupo mbele yake; Kristo ndiye sifa yake kwa sasa. Anaona ni heri kumpendeza huyu ambaye amempa uzima mpya. Amejaa na shukrani tele.
Jinsi kondoo wanavyoongozwa na mchungaji, moyo mpya nao huongozwa kwenye malisho mabichi na kando kando ya maji yaliyotulia (Zaburi 23).Anapenda kukaa karibu na Mchungaji wake Yesu na kumuandama. Lugha za dunia zinashindwa kuelezea furaha na utukufu wa moyo unaofuata nyayo za Yesu. Uhusiano na Yesu unaridhisha moyo zaidi ya kitu chochote. Anathibitisha kwamba ahadi ya Yesu ilikuwa kweli: “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami” Ufunuo 3:20.
Sasa Roho Mtakatifu, aliyechorwa kama njiwa kwenye kielelezo chetu, ameingia kuuongoza moyo huu katika ukweli wote (Yohana 16:13). Ujio wa Roho huanza kuzalisha matunda ya Roho. Matunda mazuri ya upendo, amani, furaha, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, imani, upole, na kiasi yanaonekana wazi katika moyo huu (Wagalatia 5:22,23). Upendo ulioingia kwa sasa ni kwa watu WOTE, na unamsukuma kupatana na wale aliokosana nao hapo nyuma. Utambuzi kupitia Roho Mtakatifu humwezesha Mkristo kuelewa njia impasayo kwenda na pia kutambua yale yasiyompendeza Mungu, akijiepusha nayo.
Moyo huu hutamani maziwa salama ya Neno la Mungu (1 Petro 2:2). Yeye hujifunza Neno la Mungu bila aibu na kuyashika mafundisho yake yote. Uhuru umekuja pamoja na ujasiri; haoni aibu kusema yale aliyoyaona na kusikia na kuelewa (Matendo 4:20). Kutangaza Injili hii tukufu kama mjumbe wa Kristo huleta furaha kubwa kwake.
Moyo huu unatafuta ushirikiano na watoto wa Mungu wengine. Apatapo mwili wa Kristo, yaani Kanisa la Mungu aliye hai, na mafundisho yote yanafunzwa na kudhihirishwa kwa matendo ya waumini, basi hamu ya nafsi hii inatoshelezwa (1 Wakorintho 12, Matendo 2:41).
Moyo wa Ushindi
Moyo huu ni wa ushindi. Nia yake ni kumtukuza Mungu ambaye amemwita katika ufalme wake (1Wathesalonika 2:12). Huyu mtoto wa Mungu anajitahidi kila siku kuweka kando mizigo iliomlemea, ili apige mbio ya uzima kwa uvumilivu, akimtazama Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yake (Wahebrania 12:1,2). Amejifunza kukesha na kuomba kwa sababu Shetani atamjaribu tena kwa tamaa zake. Adui huyo yuko karibu na silaha zake za giza, lakini Mkristo anayo ulinzi wa kutosha kwa kuwa amehifadhiwa na nguvu za Bwana (1Petro 1:5). Moyo huu unategemea uwezo wa Mungu pekee yake.
Mchungaji anaendelea kuongoza moyo huu kama mmojawapo wa kondoo wake. Yesu alisema, “Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua nao wanifuata; Nami nawapa uzima wa milele, wala hawatapotea kamwe, wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu” (Yohana 10:27,28). Hata Shetani hataweza kumtoa huyo kondoo mkononi mwa Mungu. Wakati mwingine anamjia kama simba avumiaye akijaribu kumkamata; wakati mwingine anamshawishi kwa ujanja kama malaika wa nuru ili ampotoshe mbali na Mlinzi wake. Hata hivyo Shetani ni lazima akimbie maadamu moyo huu ukiendelea kumpinga (Yakobo 4:7).
Moyo huu unaona hitaji la kuendelea kutakaswa zaidi akiomba pamoja na Mtunga zaburi wa zamani: “Ee Mungu unichunguze uujue moyo wangu, unijaribu mawazo yangu, uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, ukaniongoze katika njia ya milele” (Zaburi 139:23,24). Roho Mtakatifu huosha matawi ya moyo huu, akiondoa vikwazo vyake ili uweze kuzaa matunda zaidi (Yohana 15:2). Mwenye moyo huu naye anajitambua kuwa si mkamilifu, na anapofanya makosa yuko tayari kujinyenyekesha na kuomba wenzake radhi.
Mtoto wa Mungu ataona magumu; aweza kuteswa na kudharauliwa na wenzake, hata wapendwa. Msamaha na uvumilivu humwezesha azidi kuwapenda na kuwaombea ingawa wanamwudhi (Mathayo 5:44).
Njia pana ya dunia na furaha zake huja machoni na masikioni mwa msafiri huyu. Mwili unajaribiwa kupitia kupenda raha kwake, lakini mwenye moyo wa ushindi anaithamini roho yake usiokufa zaidi ya mwili wake wa uharibifu. Hakubali kutoa chochote badala ya nafsi yake. Hivyo anajikana nafsi (Luka 9:23) na kuutumikisha mwili wake (1 Wakorintho 9:27). Mungu anampigania katika mapambano yake yote.
Moyo Uliorudi Nyuma
“Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu” (Luka 9:62).
Moyo huu ni wa kuhuzunisha. Unaanza kumgeuka Mwokozi wake kutokana na uzembe na kutokufanya usafi. Taratibu moyo huu uliaanza kukataa mashauri ya Roho Mtakatifu na ya ndugu zake wa kiroho. Mungu anapoona moyo hautaki kuongozwa, hatimaye anaondoka pamoja na nguvu zake na ulinzi wake. Yanayofuata ni maadili ya Roho, kama utulivu na upole (mfano wa kondoo na njiwa); nayo yanatoka. Shetani na roho zake waovu waliofukuzwa mbele za Mungu, wamerudi tena nyumbani wasimkute. “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio wabaya kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza” (Luka 11:24-26).
Utii wa kila siku na uangalifu wa bidii ungalimlinda Mkristo huyo katika maisha yake mapya. Lakini kupitia shughuli za dunia, kuacha maombi ya kila siku, au kutokusoma Neno la Mungu, Shetani amembembeleza huyu mtoto wa Mungu alale kiroho akiwa na nia ya kwamba asiamke kamwe. “Amka wewe ulalaye” (Waefeso 5:14), ndiyo wito unaotolewa mara kwa mara na Roho Mtakatifu, lakini moyo unaorudi nyuma unazidi kusinzia tu.
Wakati mwingine mwenye moyo huu anaendelea tu kudumisha mwonekano wake wa nje wa kumpenda Mungu. Anaweza kwenda kanisani, kutoa maombi matupu, na kutoa ushuhuda. Wachungaji wasioongoka na manabii wa uongo wanaudanganya moyo huu kwa kumfariji katika hali yake, wakati hayuko tayari kuokolewa na dhambi zinazomfurahisha. Moyo wake umekuwa mgumu.
Anafanya urafiki na watu wa dunia. Vitu vya upuzi vinavyong’aa, vya anasa na hisia, vinamvutia. Maongezi ya kijinga na mzaha yanakuwa mengi. Dhamiri iliyokuwa safi imekanyagwa chini na sauti yake haisikiki tena. Malalamiko, wivu, vikwazo, kutokusamehe, na vinginevyo hutawala mawazo yake tena, zikishahidi kuwa mfalme mwovu ameshika madaraka ya moyo huu kwa sasa. Dhambi za awali zinarejea na kuchafua moyo huu, ambao ulikuwa safi na mtakatifu.
Msalaba umekuwa kikwazo, na hajikani nafsi tena. Njia za watoto wa Mungu na ushirika wao huonekana ni nyembamba na hauna thamani kwake. Mkono wa Mungu unaotuadhibu husikika kwa njia nyingi, lakini kujihurumia kumechukua nafasi ya masikitiko ya kiroho kwa dhambi. Kujihesabia haki kunatumika badala ya kuhesabiwa haki kwa imani katika Yesu Kristo.
Ee, jinsi gani hali hii ilivyo nyonge! Anasa alizofurahia kwanza hata hazimtoshelezi sasa. Lakini neema ya Mungu inazidi kumuita atubu tena.
Yesu Mchungaji wake anasikitika sana. Yuko nje akimtafuta kondoo huyu. Jioni aliwahesabu kondoo wake, na akamkosa mmoja ambaye hakurudi nyumbani. Upendo wake haukuweza kutulia. Anasihi, “Rudi, nimemwaga damu yangu kwa ajili yako”.
Mwisho wa Mwenye Moyo wa Dhambi
Muda umekwisha. Mwenya moyo wa dhambi amefikia siku ya kifo chake. Mwili wake umejaa maumivu na moyo umejaa woga. Kama kuna mali iliyokusanywa, sasa haina faida. Marafiki waliopatikana wakati wa raha sasa hawaonekani. Maovu ya dhambi yanasimama yakimshtaki moyo wa dhambi. Sheria kumi za Mungu ziletayo uzima husema wazi wakati wa kifo. Sauti ya Mungu inasema kwa mara ya mwisho, “Roho yangu kila siku haitashindana na binadamu” (Mwanzo 6:3), halafu haisikiki tena.
Sasa Roho ya Mungu humgeukia aliye hai na katika ushuhuda wa mwisho husema, “Tazama mshahara wa dhambi”. Linatisha kumtazama mwenye moyo wa dhambi wakati wa kufa. Hakuna matumaini, hakuna Mwokozi, hakuna nuru. Kuna giza na kukata tamaa tu. Kusaga meno na tanuru la moto humsubiri (Mathayo 13:42). Maangamizi haya huwasubiri wenye dhambi wote, ikiwa walikuwa hawajaacha dhambi kamwe, au ikiwa walirejea dhambi kama moyo uliorudi nyuma. “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa, hukumu” (Wahebrania 9:27).
Mwisho WA Mwenye Moyo WA Ushindi
Kwa imani Mkristo aweza kuuona mji mzuri ambao mjenzi wake ni Mungu, na ulioandaliwa kwa wale wanaompenda: MBINGUNI. Yeye humsikia Yesu akisema, “Msifadhaike mioyo, nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi, na, naenda kuwaandalia mahali….nitarudi tena na kuwapokea kwangu, ili nilipo mimi, nanyi mwepo” (Yohana 14:1-3). Mkristo anajiunga kusema pamoja na mtume Paulo, “Mauti umemezwa kwa kushindwa. U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?” (1 Wakorintho 15:54-55). Anafarijika anapokumbuka alivyosema Yesu, “Mimi ndiye ufufuo na uzima: aniaminiye ajapokufa atakuwa anaishi naye; kila aishiye kwa kumwamini hatakufa kabisa hata milele” (Yohana 11:25,26).
Amani na utulivu alizokuwa nazo katika maisha yake, zinakaa naye katika dakika zake za mwisho hapa duniani. Anapoaga, ushuhuda wa uhakika upo kwamba: kwa njia ya ukombozi katika Kristo sasa atapokea taji ya uzima. Imani hii ambayo imemhifadhi katika maisha haitamtupa katika mauti, kwa kuwa imetiwa nanga katika Mwana wa Mungu wa milele. Yesu atawatuma malaika wake kuichukua roho yake (Luka 16:22).
Mtume Yohana katika maono yake aliona “ … mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila… wamevikwa mavazi meupe… wakisema, Wokovu una Mungu wetu… na Mwana-Kondoo.” Yohana aliambiwa, “Hao ndio… wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo… Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga… Kwa maana huyo Mwana-Kondoo…atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atafuta machozi yote katika macho yao.” (Ufunuo 7:9-17)
Je, unatamani kuwepo katika mkutano mkubwa aliouona Yohana? Je, hata sasa Yesu amesimama mlangoni mwa moyo wako, akibisha? Njoo, uitikie sasa na kumkaribisha ndani. Inaweza kuwa ni mara ya mwisho kwako kusikia mwito wa Mungu.