Mungu wa Kweli Ndiye Muumbaji
Tunasoma katika Biblia, “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Na Mungu akawabarikia” (Mwanzo 1:27-28). Mungu alimwumba mwanadamu, uumbaji wake wa hali ya juu kabisa na wa hekima, “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai” (Mwanzo 2:7). Anastahili wanadamu wamtumikie na kumsifu Yeye. “Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa” (Ufunuo 4:11). Kwa hiyo, viumbe vyake vingemwabudu Yeye, na Yeye tu, “…kumwabudu katika roho na kweli” (Yohana 4:24).
Mungu aliumba dunia hii katika mazingira ya ustawi na ya kupendeza. Mimea na matunda yatokayo kwenye miti yalikuwa ni kwa ajili ya chakula cha mwanadamu (Mwanzo 1:29). Mungu wa kweli naye akapanda bustani iliyo nzuri sana iitwayo Bustani ya Edeni, na akawaweka watu wa kwanza mwanamume na mwanamke Adamu na Hawa ndani ya bustani hiyo. (Mwanzo 2:8)
Dhambi Iliingia
Mungu aliwaagiza Adamu na Hawa wasile matunda yatokayo kwenye mti wa “Ujuzi wa Mema na Mabaya” (Mwanzo 2:17). Badala ya kulitii Neno lake, wakadanganywa na Shetani kula matunda waliyoagizwa wasiyale. (Mwanzo 3) Dhambi na uvunjaji wa sheria uliingia ulimwenguni. “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi” (Warumi 5:12). Kwa kutokumtii Mungu, Adamu na Hawa walipoteza uhusiano mwema waliokuwa wakifurahia kati yao na Mungu. Kwa hiyo, ikawalazimu waondoke kwenye Bustani ya Edeni. Sasa, ikampasa Adamu afanye kazi kwa kuvuja jasho la uso wake kwa ajili ya chakula chake, na wanadamu analazimika afanye hivyo tangu wakati huo. (Mwanzo 3)
Adamu na uzao wake walihitaji Mwokozi sasa, kwa maana dhambi iliingia duniani. “Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja” (Zaburi 14:3). “Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23).
Mwokozi Ameahidiwa
Mungu wetu ni Mungu wa upendo. Hakuweza kuwaacha wanadamu bila tumaini. Pamoja na adhabu ya dhambi zao, akawaahidia Mkombozi. (Mwanzo 3:15) Kuanzia wakati huo, wanadamu wakaleta dhabihu za kondoo na mbuzi. Habili aliileta sadaka ya kwanza kama hiyo impendezayo Mungu (Mwanzo 4:4). Sadaka hizi ziliwakilisha mtu Yesu ambaye ni kama “Mwana kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu” (Yohana 1:29). Yesu aliacha makao yake Mbinguni na utukufu wa Baba yake, na alikuja ili atufie msalabani kama upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16). Yesu alijitoa kama dhabihu ya mwisho kwa kumwaga damu yake mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu (Waebrania 9:12 na 16). Ni lazima tumtazamie Yesu kwa imani. “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Mdo 4:12).
Je, Mungu Anataka Mwanadamu Amwabudu Yeye?
Mungu alitia utashi wa kuabudu katika mioyo ya wanadamu. Hatuwezi kumwona Mungu. Yesu amesema “Mungu ni Roho” (1 Yohana 4:24). Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. (1Yohana 4:12) Lakini kwa macho ya kiroho tunaweza tukamtazama, “...kama amwonaye yeye asiyeonekana” (Waebrania 11:27). Baba yetu wa mbinguni anawatafuta waabudu hao watakaomwabudu Baba katika Roho na kweli. (Yohana 4:23) Yesu asema, “Imeandikwa, msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake” (Mathayo 4:10). Katika 2Wafalme 17:36, twasoma, “...yeye ndiye mtakayemcha, yeye ndiye mtakayemsujudia, yeye ndiye mtakayemtolea sadaka”. Katika Zaburi tunasoma mengi kuhusu kumtukuza Bwana, kumtumikia na kumwabudu yeye, na kumtolea sadaka za kuteketezwa. Katika Zaburi 103:1-2 twasoma, “ Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote.”
Je, Mungu Anaonya Dhidi ya Miungu, na Kukataza Ibada ya Sanamu?
Anasema: “Mimi ni Bwana Mungu wako... Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchongwa, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu…” (Kutoka 20:2-5). “Kwa maana hutamwabudu mungu mwingine...” (Kutoka 34:14). Mtume Paulo asema, “...haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu” (Mdo 17:29). Katika Wafilipi 2:9-11 twasoma, “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; Ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Tofauti Kati ya Mungu wa Kweli na Sanamu
Mtume Paulo asema hivi: “...twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu. Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu” (1Wakorintho 8:4-5). “Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, alitakalo lote amelitenda. Sanamu zao ni fedha na dhahabu, kazi ya mikono ya wanadamu. Zina vinywa lakini hazisemi, zina macho lakini hazioni, zina masikio lakini hazisikii, zina pua lakini hazisikii harufu, mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, wala hazitoi sauti kwa koo zao. Wazifanyao watafanana nazo, kila mmoja anayezitumainia” (Zaburi 115:3-8). Katika Yeremia 32:17-19, Nabii asema hivi, ”Aa! Bwana Mungu, tazama wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza….Mungu aliye mkuu, aliye hodari, Bwana wa majeshi ndilo jina lake; mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.”
Wakati Israeli ilipotenda dhambi na ibada ya sanamu ilipoanzishwa, Mungu alimwita nabii wake Eliya kuhubiri dhidi ya ibada ya sanamu. Katika 1Wafalme 18, tunayo habari ambayo nabii ya kweli Eliya, alishindana na manabii mia nne na hamsini wa Baali (sanamu yao). Alisema Mungu ambaye atajibu kwa moto atatambuliwa kuwa ndiye Mungu wa kweli. Manabii wa Baali walimwita mungu wao tangu asubuhi hata jioni, “...lakini hapakuwa na sauti; wala aliyejibu, wala aliyeangalia” (mstari wa 29).
Eliya, aliomba akisema, “Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo, moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayalamba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji” (mistari 37-38).
Wakati wale Wafilisti mapagani walipokuwa wamelichukua “Sanduku la Mungu” ambalo liliwakilisha uwepo wa Mungu, wakalitia katika nyumba ya sanamu yao, nyumba ya Dagoni. “Hata walipoamka kesho yake asubuhi, kumbe! Dagoni ilikuwa imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana; na kichwa chake Dagoni na vitanga vya mikono yake vyote viwili vimekatika, vipo vimelala kizingitini; Dagoni ikasalia kiwiliwili chake tu” (1Samweli 5:4).
Kumwitia Mungu wa Kweli
“Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau” (Zaburi 51:17). “Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake, na amrudie Bwana, naye atamrehemu; an arejee kwa Mungu wetu, naye atamsamehe kabisa” (Isaya 55:7). “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako” (Mdo 16:31). “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa wototo wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie” (Mdo 2:39). “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami” (Ufunuo 3:20). Je, unamsikia Yeye akibishia mlango wa moyo wako? Je, utamkaribisha aingie? Nakusihi ufanye hivyo.