Kila mahali watu wote hutamani kuwa na vitu vya kupendeza kwa maisha yao. Kila mmoja angependa kuwa na chakula kizuri, na cha kutosha kugawanya kwa marafiki na wageni; nguo zilizokamilika, na za kutosha kubadili kwa wakati mbalimbali; nyumba nzuri, imara na kubwa ya kutosha, yenye paa nzuri kwa majira yote.
Pia tunatarajia kuwa na kiasi cha fedha mkononi ili kukabili matumizi yote, shughuli zetu, kwa dawa ukijitokeza ugonjwa, na hata ya kutosha kusafiria kuwaona marafiki mahali pengine. Kila mmoja hutaka dhamana ya kufanikiwa, hata kuwa na pesa za ziada mkononi kumaliza shida za dhorura.
Katika Mathayo 6:32, Yesu alisema kuhusu uelewa wa Mungu kujua mahitaji yetu. Pia katika Luka 12:30 “……lakini Baba yenu wa mbinguni ajua ya kuwa mna haja na hayo”.
Katika Maandiko Matakatifu, hamna neno lolote juu ya Mungu wetu kuweka tofauti yoyote kwa makabila, mataifa, au rangi za watu mbalimbali. Katika mpango wake wa busara, Mungu alijua watu wote wanahitaji riziki sawa. Mungu ameuweka uwezekano wa kupata mahitaji haya kwa maisha, hata anao mpango maalum kwa ajili ya kila mmoja wetu.
Sababu kubwa kwa mahitaji yetu kutokutimizwa siyo kosa la Mungu, wala tusingelaumu mazingira yetu. Wala siyo kosa la watu karibu nasi. Lakini wengi huteseka na kusumbuka katika maisha na hawajui sababu ya kushindwa.
Watu wengi sana wanaendelea kutumia njia mbaya ili kupata mahitaji ya maisha... lakini kwa nini mtu atarajie matokeo mema kutokana na njia mbaya??? Mungu alisema, “fanya kazi siku sita, na ufanye kazi zako zote” (Kutoka 20:9). Hata Mungu hatarajii kwamba mtu mvivu au asiyemwaminifu kupata chakula cha kutosha. Je, KWA NINI sisi tutarajie???
Ikiwa hatupendi kufanya kazi zetu vizuri siku sita kwa juma, na tusitegemee kupata vitu vinavyopendeza. Wala tusingefikiri kwamba kuomba chakula, au hela, kungeleta heshima na maendeleo kutoka kwa mtu yeyote.
Unapokuwa mzembe katika kazi yako wakati msimamizi wako haoni, unampunja. Usitarajie kwamba utakapowaajiri vibarua wako watakufanyia kazi vizuri. Tabia yako isiyoonekana hujulikana kabisa kwa Mungu wetu asiyeonekana. Huyu Mungu atatulipa kwa matendo yetu. Twasoma katika Kumb. 32:35 na pia katika Warumi 12:19 kwamba kisasi kwa matendo yetu maovu kitatoka kwake.
Mtihani wetu wa kwanza wa kuonyesha kama tunastahili mafanikio au la, huanzia mwanzo wa maisha yetu; ni katika utii wetu kwa baba na mama. Tukishindwa katika zoezi hili la kwanza ambayo ni muhimu sana, hatuna ahadi ya ushindi katika maisha. Tusome Kumb. 5:16: “Waheshimu baba na mama yako, kama Bwana Mungu wako alivyokuamuru; siku zako zipate kuongezeka; nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo, na Bwana Mungu wako”. Tusome pia Waefeso 6:1-3. “Watoto watiini wazazi wenu katika Bwana; maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba na mama; amri hii ndiyo ya kwanza yenye ahadi; upate heri ukae siku nyingi katika dunia”. Kuwalaani wazazi huleta kifo. Tazama Kutoka 21:17. “Yeyote amlaaniye baba yake na mama yake, hakika atakufa”.
Zoezi la pili ni katika uaminifu kwa msimamizi wako aliyekuajiri. Ukimdanganya, kama ni rafiki yako, adui, au serikali, usitazamie kupata maendeleo. Hata kama msimamizi wako hana habari kwamba unatumia vifaa au muda vibaya, lakini, lazima tujue kwamba Mungu Mkuu wa mbinguni anaandika matendo yetu na tabia zetu. Katika Biblia, Hesabu 32:23 tunasoma: “……. Nanyi jueni hizo dhambi zenu zitawafichua”. Katika Luka 12:2 Yesu alisema: “Kwa maana hakuna kilichofunikwa ambacho hakitafunuliwa: wala kilichofichwa ambacho hakitajulikana”. Katika Luka 16:12 Yesu ameliweka wazi zaidi. Alisema: “Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, Je, nani atawapa kilicho chenu?” Tusitarajie kujipatia chochote ikiwa kwa namna yoyote tumekuwa watu wasio waaminifu katika mali, muda, au vifaa vyake. Bali, ni lazima kwa unyoofu tusaidie kuendeleza biashara ya msimamizi wetu ambaye anatulipa mshahara, kabla hatujatazamia yaliyo mema kwetu.
Kama umeahidi kulipa; kama umeahidi kuja kufanya kazi; kama umeahidi kurudisha ulichoazima; kama umeahidi lakini hukutimiza ahadi yako: Usitarajie kwamba Mungu atakuahidi yaliyo mema. Kama maneno yako hayawezi kuaminiwa, usitegemee kwamba utafanikiwa. Au kama kwa namna yoyote unatamka uongo; unaeleza maelezo ya uongo, usiwe na matumaini ya kuambiwa ukweli. Fikiria mwisho wa waongo…. Katika agano jipya, katika Ufunuo 21:8, tunasoma: “…….na waongo wote, sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto na kiberiti.”
Watu ambao wanaona ni rahisi kuchongea uongo, pia wanaweza kuona ni rahisi kuiba. Kama wewe ni mwizi, pia unaweza kuwa na tumaini la kuibiwa na wezi wengine. Katika 1Wakorintho 6:10 twasoma: “....wala wezi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi hawataurithi ufalme wa Mungu.”
Au kama umepata fedha kwa njia rahisi na za haraka kwa njama ya faragha na ya kibinafsi, usiwe na matumaini ya kuitunza. Wewe siyo mwerevu sana kwa jinsi unavyofikiria. Katika Methali 13:11 twasoma: “Mali iliyopatikana kwa njia isiyofaa itapunguzwa; lakini yeye apataye kwa kufanya kazi atazidishiwa.” Tunaweza kutarajia biashara ya “kuwa tajiri haraka” kuishia “kuwa maskini haraka.” Methali 28:22 husomeka: “Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri; wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.”
Na tutazame dhambi ya kupokea rushwa---- kuchukua au kutoa pesa isiyo halali au zawadi kinyume cha utaratibu ili uwe na msimamo wa kupendeza. Kama uko katika cheo chenye mamlaka na uwezo, au la, hii ni dhambi ya kuchukiza ambayo huhesabiwa na dhambi zingine za mauti. Tusome Zaburi 26:9-10: “Usiiondoe nafsi yangu pamoja na wakosaji, wala uhai wangu na watu wa damu: ambao mikononi mwao mna madhara, na mkono wao wa kuume umejaa rushwa.” Na tena katika Amos 5:12 twasoma, “Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; nanyi mnawaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao.” Pia tunasoma hivi katika Kutoka 23:8: “Nawe usipokee rushwa, kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na huyapotoa maneno ya wenye haki.” Kama tunachukua rushwa kutoka kwa mtu yeyote au dhidi ya mtu mwingine, nasi tutegemee kwamba wengine watachukua rushwa juu yetu. Ufisadi ndio adui mbaya dhidi ya maendeleo, katika jamii na vile vile katika taifa.
Usitegemee kwamba elimu au hata mafunzo ya chuo yataepusha mtu asihusike na ufisadi na maovu. Ni mabadiliko ya moyo pekee kupitia damu ya Yesu Kristo unayoweza kutukomboa kutokana na maovu na uhalifu uliojifichia.
Ukimtakia adui yako maovu, usitegemee jambo lolote lingine isipokuwa kwamba matakwa yako mabaya dhidi yake yatakurudia wewe mwenyewe. Soma Zaburi 35:7-8, “Maana bila sababu wamenifichia wavu, bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafla: na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe: na uharibifu aanguke ndani yake.”
Ikiwa umepigana au kugombana na wengine, usitumainie amani maishani mwako. Msukosuko na woga utakufuata haraka hata utakapofanya mapatano ya amani.
Kama umeokota vitu au hela ya mtu iliyopotea, usiichukue kama pato lako. Ikiwa hutajitahidi kwa unyoofu kurudisha kilichopotea kwa aliyeipoteza, usiwe na tumaini kwamba vitu vyako vilivyopotea vitarudishwa kwako.
Usitarajie mali ya rafiki yako tajiri kukusaidia. Pesa zake zaweza kutoweka na ninyi nyote mtasikitishwa. Itakuwa bora upate za kwako. Katika Methali 11:28 twasoma, “Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani.”
Haitakiwi kuwafundisha watoto wadogo kuombaomba hela kutoka kwa wengine. Yaweza kuwa kitendo hiki hakina madhara kwa mtoto, lakini bila shaka itageuka kuwa tabia mbaya akiwa mtu mzima. Afadhali kwa unyenyekevu tuikubali hali ya maisha pamoja na mahangaiko yake na kuamua kwenda kufanya kazi siku sita kwa juma. Na tujifundishe sisi na watoto wetu namna ya kutoa badala ya kuomba ili kupewa kitu bure. Katika 2Wakorintho 9:6-8, Mtume Paulo anaandika juu ya jambo hili--- “Lakini nasema neno hili, apandaye haba atavuna haba, na apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kwa kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema.” Yesu alifundisha kwamba ni bora kutoa kuliko kupokea (Matendo 20:33-35).
Ikiwa yeyote ni mzembe na anakataa kufanya kazi, na kisha badala yake anachagua kuwa mhubiri au mchungaji, au kujifanya kuwa nabii, pasipo kuchaguliwa na Mungu na watu wa Mungu kumchagua, na akatumaini watu kumlipa........ asiwe na matarajio kwamba mwisho wake utakuwa mzuri. Hakuna wingi wa mahubiri wala utabiri utakaofunika siri ya uzembe. Utabiri wa uongo utaleta tu laana hata kama imebuniwa kwa hila. Tusome katika 2Petro 2:1-3: “Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. Na wengi watafuata ufisadi wao, na kwa hao njia ya kweli itatukanwa. Na katika kutamani (tamaa ya pesa na sifa) watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.”
Tusitegemee kuvuna yaliyo bora zaidi ya tuliyopanda. Kama humsaidii asiye na namna au mjane, usitegemee msaada wakati siku yako ya mateso itakufikia. Kama hupendi kuwasaidia wazazi wako katika uzee wao, usitazamie kwamba jamaa yako watapenda kukusaidia katika uzee wako. Tusome Methali 21:13: “Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, yeye naye atalia, lakini, hatasikiwa.” Na tena katika Wagalatia 6:7,8: “Msidanganyike; Mungu hadhihakiwi; Kwa maana cho chote apandacho mtu ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa roho, katika roho atavuna uzima wa milele”.
Tusidhani kwamba hatuwezi kusitawi mpaka yaje maendeleo ya jamii ya kisasa. Watakatifu na watu wa Mungu wa zamani hawakusubiri mapato mengi. Mungu aliwabariki ijapokuwa waliona magumu na taabu, kwa rafiki na adui; palipotokea mvua au ukame; palipotokea mavuno mengi au madogo. Hakuna kinachoweza kuzuia ushindi endapo tutakuwa katika mapenzi ya Mungu. Ingawa kutatokea wakati wa kujaribiwa, au hata dhiki; Mungu atafariji na kusaidia.
Lakini tukumbuke kwamba ahadi zisizotimizwa zinakuwa uongo.
Udanganyifu na ujanja unakuwa wizi.
Chuki na ugomvi unakuwa uuaji.
Kuishi katika ufisadi na dhambi huleta msiba katika maisha---- na bila kuitubu italeta hukumu ya Mungu na maangamizi ya milele siku ya mwisho. Mtu mwaminifu atataka kukumbuka na kutekeleza ahadi zake kwa uangalifu, hata kama anakuwa na hali ngumu sana kuliko alivyofikiria wakati ule alipokuwa akitoa ahadi hiyo. Kwa njia hiyo hatokei kuwa mwongo. Mnyoofu wa Mungu hatalaghai, hata kama anayo nafasi ya siri kufanya hivyo--- Kwa njia hiyo hawatakuwa wezi.
Wale wenye moyo uliojaa upendo wa Mungu (upendo kwa kila mmoja) wataepuka mawazo mabaya, ugomvi, na mapigano----Kwa njia hiyo hawatakuwa wauaji.
KUISHI KWA KUFUJA HULETA HUZUNI NA UPUNGUFU MWINGI!
Ikiwa umepata kidogo au nyingi; kama umekuwa mshindi kwa kiasi kidogo au kikubwa; kama umekitumia kwa kununua vitu vya tamaa yako au anasa, au umekitumia katika kamari au michezo ya bahati (nasibu), usiwe na matumaini ya kupata hela ya kutosha wakati mahitaji muhimu yametokea. Katika Methali 21:17, twasoma: “Apendaye anasa atakuwa maskini: apendaye pombe na mafuta hatakuwa tajiri.”
Usitarajie kupata mafanikio katika njia yoyote ile kwa kurekebisha tabia yako, isipokuwa kupitia upendo wa Yesu unaokomboa. Jitoe KWAKE. Funua, tubu, ungama dhambi zako za nyuma. Usitegemee nguvu zako, sifa, au kazi zako njema. Binadamu anashindwa kabisa pasipo Kristo.
Wala hamna tumaini kwamba mtu maarufu au mganga wa kienyeji aweze kukuwekea mambo yako sambamba na unavyopendelea. Maaguzi na ubashiri wa mchawi hazina nguvu za kumletea yeyote mafanikio. Gharama ya kutoa kafara ni hasara tena.
BALI--
Tunaweza kumtumaini Mungu Mkuu wa mbingu na nchi, kututimizia ahadi zake njema, ikiwa tutafuata mipango YAKE kwa kujinyenyekea. Kama tutatubu na kuongoka, kutakuwa na tumaini. Hamna ahadi, hata moja itakayopungua KWAKE. Tusome alichosema Mfalme Daudi katika Zaburi 37:17-28: “Maana mikono ya wasio haki itavunjika, bali Bwana huwategemeza wenye haki. Bwana anazijua siku za wakamilifu, na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, na siku za njaa watashiba. Bali wasio haki watapotea, nao wamchukiao Bwana watatoweka, kama uzuri wa mashamba, kama moshi watatoweka. Asiye haki hukopa wala halipi, bali mwenye haki hufadhili, hukirimu. Maana waliobarikiwa na yeye watairithi nchi, nao waliolaaniwa na yeye wataharibika. Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana, naye aipenda njia yake. Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza. Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, lakini sijamwona mwenye haki ameachwa wala mzao wake (watoto) akiomba chakula. Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, na mzao wake (watoto) hubarikiwa. Jiepushe na uovu, utende mema, na kukaa hata milele. Kwa kuwa Bwana hupenda haki. Wala hawaachi watauwa. Wao hulindwa milele, bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.” Tena tusome Methali 19:17: “Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana; naye atamlipa kwa tendo lake jema.”
Kama tukimrudia Mungu kwa moyo wote, na kupata msamaha wa dhambi zetu kwa kutubu, na kujituma kwa mpango wa Bwana, na kulinda amri zake, na tumefanya kazi siku sita za juma, na tumeridhisha vizuri mahitaji ya familia yetu, na tumetoa kwa maskini na kwa kazi ya Bwana, na tumekuwa waaminifu kwa wengine na kwa mali yao---- ndipo pia itawezekana kulinda amri yake ya mwisho katika jambo hili. Tusome Mathayo 6:31-33: “Msisumbuke, basi mkisema, tule nini? Au tunywe nini? Au tuvae nini? Kwa maana hayo yote mataifa huyatafuta; Kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; NA HAYO YOTE MTAZIDISHIWA.”