Kabla ya muda haujakuwepo Mungu alikuwepo. Aliumba dunia na kila kitu kilichomo. Katika upendo wake, Mungu akaumba mwanadamu kwa sura yake mwenyewe akawaweka kwenye bustani nzuri. Wanadamu hawakutii maelekezo ya Mungu. Kutokutii huku kulikuwa ni dhambi iliyowatenganisha mbali na Mungu. Aliwaambia kwamba wanapaswa kutoa dhabihu za wanyama wadogo wasio na madoa yoyote kwa ajili ya dhambi zao. Dhabihu hizi hazikulipia dhambi zao bali zilielekeza dhabihu ya mwisho ambayo Mungu angetoa. Siku moja Mungu angetuma mwanawe Yesu duniani awe dhabihu ya mwisho.
Yesu na Malaika
Miaka elfu nne baadaye, katika mji wa Nazareti aliishi mwanamke kijana aliyeitwa Mariamu. Naye alikuwa amechumbiwa na Yusufu. Siku moja malaika akamtokea Mariamu akampasha habari kwamba atamzaa mtoto maalumu. Atapaswa kumwita Yesu. Mtoto huyu asingekuwa na baba wa kidunia.
Kuzaliwa kwa Yesu
Baada ya ziara ya malaika, Yusufu na Mariamu walisafiri Bethlehem ili kulipa kodi zao. Walipofika Bethlehem, mji ukawa na watu wengi. Wakalala usiku katika zizi la wanyama. Wakakesha usiku katika zizi la wanyama kwa sababu hakukuwa na nafasi katika nyumba ya wageni. Hapo ndipo Yesu alipozaliwa. Mariamu akamvika nguo za kitoto na akamlaza horini.
Wachungaji
Usiku ule ule, milimani nje ya mji, wachungaji walikuwa wakichunga mifugo yao. Malaika akatokea na utukufu wa Mungu ukawaangazia wachungaji pande zote. Naye malaika akasema, “Msiogope kwa maana nawaleteeni habari njema ya fuhara kubwa itakayokuwa kwa watu wote. Usiku wa leo, Mwokozi amezaliwa. Naye ndiye Kristo Bwana. Mtamkuta akivikwa nguo za kitoto akilala horini. Ndipo malaika wengi wakatokea wakitukuza na kumsifu Mungu, wakisema “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” Baada ya malaika kuondoka, wale wachungaji wakawaacha kondoo zao nao wakaenda kwa haraka Bethlehem. Pale walimkuta mtoto kama walivyoambiwa na malaika.
Mamajusi
Baada ya kuzaliwa Yesu, mamajusi wakafika Yerusalemu kutoka nchi nyingine. Wakauliza, “Yuko wapi mtoto yule Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake kutoka mashariki nasi tunataka kumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia hayo, akafadhaika. Akawaita makuhani na walimu wa sheria waje kwake. Walimwambia kwamba manabii walikuwa wamesema mfalme angezaliwa Bethlehem. Mfalme Herode akawatuma mamajusi kule Bethlehem kumtafuta huyo Mfalme. Wakati mamajusi walipoondoka Yerusalemu, ile nyota ikawaongoza hadi nyumba walipompata mtoto Yesu. Wakamsujudia na kumwabudu, wakimpa zawadi za dhahabu, ubani na manemane. Mungu akawaonya mamajusi wasirudi kwa yule mfalme mwovu Herode, hivyo wakapita njia nyingine.
Sababu ya Zawadi yake Mungu
Yesu alikuwa Mwana wa Mungu. Aliishi bila kutenda dhambi na akawa mkamilifu katika namna zake zote. Alipofika umri wa miaka thelathini, Yesu akaanza kufundisha watu habari za Mungu, Baba. Akafanya miujiza mingi kama vile kuwapa vipofu kuona, kuponya magonjwa, na hata kufufua wafu. Zaidi ya yote, akafundisha namna ya kupata uzima wa milele Mbinguni. Kisha akautoa uhai wake kama dhabihu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.
Biblia inasema katika Yohana 3:16, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yesu alikuja duniani ili afe msalabani kama dhabihu kuu. Kupitia kifo chake, malipo ya dhambi zote yamelipwa. Hakuna haja tena kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Huu ulikuwa utimilifu wa ahadi ya Mungu kutuma Mwokozi. Ijapokuwa Yesu aliuawa na watu waovu, mauti hayakuwa na nguvu juu yake. Baada ya siku tatu akafufuka mshindi kutoka kaburini. Katika siku zilizofuata ufufuo wake, Yesu akaonekana na wengi. Basi siku moja, baada ya kuwabariki wafuasi wake, akapaa Mbinguni.
Tunapochagua kuamini na kuyatoa maisha yetu kwa Yesu, damu yake hututakasa kutoka dhambi zetu. Tunapokubali zawadi hii ya wokovu, tunaunganishwa tena na Mungu. Yesu anakuwa Mwokozi wetu binafsi, na tunaweza kufurahia baraka za kuwa watoto wake! Siku moja Yesu atakuja tena. Atapeleka waumini wote wa kweli Mbinguni. Pale wataishi milele pamoja na Mungu.
Tazama, Mwana-kondoo aichukuaye dhambi ya ulimwengu.–Yohana 1:29